Zungu afunguka siri ya kumzima Michael Joseph

KIPA wa zamani wa Fufuni, Idrissa Zungu, amemtaja mshambuliaji wa KVZ, Michael Joseph kama mchezaji aliyemsumbua zaidi kwenye Ligi Kuu Zanzibar wakati walipokutana.

Zungu ambaye kwa sasa anaitumikia KVZ aliyojiunga nayo msimu huu katika usajili wa dirisha dogo akitokea Fufuni, amesema jambo kubwa lililokuwa linamtatiza ni aina ya uchezeji wa mshambuliaji huyo ambapo hujui wakati gani anashambulia.

Mbali na hilo, Zungu amesema anatamanai kuendelea kucheza naye kwani anapompigia mipira mirefu, ana unawezo wa kusababisha hatari kwa wapinzani.

“Napenda kuwa kikosi kimoja na Michael kwa sababu ni aina mchezaji ambaye anajituma zaidi na mwenye kuipambania timu kupata matokeo mazuri,” amesema Zungu.

Wakati huohuo, Zungu amekumbushia alivyokutana na mshambuliaji huyo katika duru la kwanza la Ligi Kuu Zanzibar ambapo Fufuni iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya KVZ.

Amesema, katika mchezo huo aliokoa shambulizi la kushtukiza kutoka kwa Michael aliyepiga mpira kwa mtindo wa kubinuka ‘tik-tak’ ambapo kwa bahati nzuri alimuona akijiandaa kufanya hivyo, ikawa rahisi kukoa.

Kipa huyo amewaomba mashabiki wa KVZ kujitokeza uwanjani kuwapa hamasa wanapocheza mechi za ligi na wakipata matokeo mazuri washkuru lakini ikitokea tofauti, wasikate tamaa.

Zungu ambaye tangu ametua kikosini hapo amedaka mechi moja ya ligi dhidi ya Mafunzo huku Bashir Muslim Darueshi akiwa ndiye kipa namba moja kikosini hapo, amesema kama ingetokea asingekuwa mchezaji mpira, basi angekuwa mwanasarakasi kwani ni miongoni mwa mchezo anaoupenda zaidi.