Mimea vamizi yaathiri maeneo ya malisho nchini

Arusha. Jamii za kifugaji zimetakiwa kuboresha usimamizi wa malisho ili kufufua afya ya nyanda za malisho na kupunguza kiwango cha hewa ukaa angani.

Hayo yamebainishwa leo, Jumamosi Aprili 11, 2026 na Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Maeneo ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Wanyama kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Asimwe Rwiguza, katika mkutano wa wadau uliojadili mradi wa hewa ukaa kwa jamii zinazoishi katika nyanda za malisho wa Enjipai, unaolenga kuboresha maeneo ya malisho kupitia biashara ya kaboni.

Amesema changamoto kubwa zinazoikabili sekta ya malisho nchini ni pamoja na uharibifu wa ardhi na mimea vamizi, huku akisisitiza umuhimu wa mradi huo unaolenga kuboresha malisho na kuinua kipato cha wafugaji kupitia biashara ya kaboni.

Amesema hali hiyo imekuwa ikiathiri upatikanaji wa malisho bora kwa mifugo na hivyo kudhoofisha sekta ya ufugaji.

“Maeneo mengi ya malisho hayatoi tija kama ilivyokusudiwa kutokana na changamoto hizo. Mimea vamizi na vichaka vimeongezeka, hali inayosababisha kupungua kwa nyasi bora kwa ajili ya mifugo,” amesema.

Amesema kupitia mradi huo, wafugaji wanatarajiwa kupata fursa ya kuboresha maeneo yao kwa kuondoa mimea vamizi, kupunguza vichaka na kuongeza mbegu katika maeneo yenye upungufu wa malisho.

Dk Asimwe ameeleza kuwa hatua hizo zitasaidia kuongeza uzalishaji wa malisho ya kutosha kwa mwaka mzima na kupunguza utegemezi wa wafugaji kuhama-hama kutafuta malisho wakati wa ukame.

Awali, Meneja Mradi wa Shirika la Kuhifadhi Mazingira la The Nature Conservancy (TNC), Charles Masawe, amesema wanashirikiana na Serikali katika kuendeleza nyanda za malisho, na kuwa katika mradi huo wanashirikiana na wadau wengine kutekeleza mradi huo katika wilaya tatu.

Amesema vijiji 49 vya wilaya hizo ambazo ni Longido (11), Monduli (17) na Simanjiro mkoani Manyara (21), vitanufaika na mradi huo ambao umelenga kuwezesha jamii ya wafugaji kumiliki na kusimamia kwa njia endelevu maeneo yao ya malisho.

“Lengo lingine ni kuwezesha upatikanaji wa malisho kwa ajili ya mifugo yao, kuwezesha jamii kunufaika na mapato ya kaboni ambapo kupitia fedha hizo wataweza kufanya miradi ya maendeleo.

“Mradi utawezesha kusimamia maeneo yao ya malisho, hasa ikizingatiwa jamii hii inategemea ufugaji kama shughuli yao kubwa ya kiuchumi, na tunaamini maeneo yao yakisimamiwa na kuboreshwa yatatoa tija na kuwa na malisho msimu wote wa mwaka ili waondokane na adha ya kuhama-hama,” amesema.

Ameongeza kuwa mradi huo ambao uko katika hatua ya awali unatarajiwa kuanza mwaka huu baada ya vijiji kuingia mikataba ya utekelezaji, ambapo utatekelezwa kwa kipindi cha miaka 40 hadi mwaka 2066.

“Ndiyo maana tuko hapa kujadiliana na wadau na wawakilishi wa wananchi ili kuelimishana na kupata maoni ya kuboresha mradi huu. Tukiangalia maeneo mengine, miradi ya kaboni imesaidia wananchi kutumia sehemu ya mapato yao kutoa ufadhili kwa wanafunzi ambao familia zao hazina uwezo,” amesema.

Amesema maeneo mengi ya malisho yameharibika na kughubikwa na ulishaji wa mifugo uliopita kiasi na kusababisha mmomonyoko mkubwa wa ardhi, hali inayochangia maeneo hayo kutokuwa na tija ya kuzalisha nyasi au malisho yanayofaa kwa mifugo yao.

Kwa upande wake, mwanajamii kutoka Simanjiro, Sarah Alakara amesema mradi huo ni fursa muhimu lakini bado unahitaji uelewa mkubwa kwa wananchi ili kuondoa hofu kuhusu umiliki wa ardhi.

“Wananchi wengi wana wasiwasi kuwa miradi kama hii inaweza kuondoa umiliki wao wa ardhi, hasa kutokana na uzoefu wa nyuma ambapo maeneo yalibadilishwa kuwa hifadhi,” amesema.

Amesisitiza umuhimu wa kutoa elimu ya kutosha kwa jamii ili kuelewa kuwa mradi huo hautachukua ardhi yao bali utasaidia kuiboresha na kuwanufaisha kiuchumi,” amesema.