Jumanne Elfadhil awashusha presha Tanzania Prisons

BEKI na nahodha wa zamani wa Tanzania Prisons, Jumanne Elfadhil, amesema katika mechi 12 za Ligi Kuu Bara zilizobaki kwa timu hiyo, lolote linaweza kutokea, hivyo wachezaji wa kikosi hicho wanapaswa kujiamini kila wanaposhuka dimbani.

Elfadhil aliyeitumikia timu hiyo kwa takribani miaka 14, kwa sasa anaendelea na majukumu yake ya ajira kwenye Jeshi la Magereza baada ya kutangaza kutundika daruga tangu msimu uliopita.

Kauli yake hiyo imekuja ikiwa hivi sasa Tanzania Prisons haipo kwenye wakati mzuri katika Ligi Kuu Bara ikishika nafasi ya 15 ikikusanya pointi 13 ikicheza mechi 18, zimebaki 12 kumaliza msimu.

Amesema anaumizwa na matokeo ya timu hiyo akieleza kuwa kinachopaswa kufanyika ni wachezaji kujiamini, kuzungumza uwanjani na kujitolea kadri wawezavyo.

Kwa Elfadhil, anaamini mechi 12 zilizobaki kama wachezaji wakikaza, basi timu inaweza kubaki salama, akibainisha kuwa tatizo lililowakuta la kuhamahama uwanja, ratiba ngumu na maingizo mapya kikosini.

“Kuna muda wachezaji hawazungumzi uwanjani, nakumbuka enzi zangu Ivo Mapunda alikuwa akitukosoa nikiwa na David Mwantika, hivyo basi wachezaji wajiamini kwa sababu walishafungwa, walishatoa sare na hata kushinda.

“Mechi 12 ni nyingi, wakikaza wanaweza kutoboa kwani unaona kwa sasa ujio wa kocha Shadrack Nsajigwa umeongeza kitu, timu inacheza na unaona inahitaji kitu, binafsi sijaikatia tamaa na lolote linawezekana,”€  amesema.

Katika hatua nyingine, Elfadhil amebainisha kuwa, tangu aanze kucheza soka hadi kustaafu, hajawahi kuona Ligi Kuu Bara inayochezeshwa kwa haki kama ilivyo msimu huu, akieleza kuwa kama ingekuwa hivi miaka yote, huenda timu yoyote ingetwaa ubingwa.

“Ligi ya msimu huu imebadilika sana, waamuzi wanachezesha kwa haki, timu yoyote inapata matokeo mazuri popote na kwa mpinzani yeyote, ingekuwa imefanyika hivi hata miaka ya nyuma, bingwa angekuwa anabeba yeyote,” amesema Elfadhir