Dar es Salaam. Wakati jitihada za kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza zikiongezeka nchini Tanzania, hatua mpya imepigwa baada ya kuzinduliwa kwa kitabu kitakachotumika kufundishia somo la saratani kwa wanafunzi wa shule za msingi.
Kitabu hicho kilichopewa jina la Amani Rafiki Shujaa, kimeandikwa na Baraka Fundo ambaye ni mtaalamu wa fizikia tiba katika kitengo cha nyuklia tiba cha Taasisi ya Saratani Ocean Road jijini Dar es Salaam, kikilenga kutoa elimu ya mapema kuhusu saratani na njia za kujikinga kwa watoto na jamii.
Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika leo Jumamosi, Aprili 11, 2026, Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Dk Suleiman Ikomba, amesema afya na elimu ni mihimili miwili isiyoweza kutenganishwa katika kujenga Taifa imara.
“Afya na elimu katika maisha ya binadamu ukivitenganisha kuna mahali hapatakuwa sawa,” amesema.
Ameeleza malezi bora ya watoto yanahitaji mchango wa walimu na wataalamu wa afya kwa pamoja ili kuhakikisha jamii inafikia maendeleo yenye tija.
Dk Ikomba ameshukuru mamlaka za elimu nchini kwa kukiidhinisha kutumika rasmi shuleni kuanzia darasa la tatu hadi la sita, hatua inayolenga kuwajengea wanafunzi uelewa wa awali kuhusu magonjwa yasiyoambukiza wakiwa katika umri mdogo.
Katika hatua nyingine, Dk Ikomba amempongeza mwandishi wa kitabu hicho, Baraka Fundo, kwa juhudi zake za kuandaa nyenzo ya kielimu itakayosaidia watoto na wazazi kuelewa hatari ya saratani.
“Kitabu hiki kitawajengea uelewa wa mapema watoto wetu na wazazi juu ya maradhi ambayo kwa Taifa imekuwa ni vigumu kuyazungumzia,” amesema.
Ameongeza dunia ya sasa inakabiliwa na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza, akisisitiza umuhimu wa elimu ya mapema katika kupambana nayo.
“Ndugu yetu Fundo ameanza na saratani, lakini tunahitaji vitabu zaidi kuhusu kisukari, lishe duni na changamoto nyingine za kiafya,” amesema.
Dk Ikomba amesisitiza uwekezaji kwa walimu kuwa ni njia bora ya kufikisha maarifa kwa jamii.
“Ukitaka kuisaidia jamii ipasavyo, wekeza kwa walimu. Mtuletee tufundishe watoto wetu wakiwa wadogo,” amesema.
Kitabu hicho kimepitiwa na wadau mbalimbali wa elimu na afya, kimehaririwa na Dk Clement Mubanga na kutafsiriwa na Baraza la Kiswahili la Taifa ili kuendana na viwango vya kitaifa.
Kwa upande wake, Baraka Fundo amesema msukumo wa kuandika umetokana na uzoefu wake katika kuwahudumia wagonjwa wa saratani.
“Nimeona namna jamii inavyopata shida na saratani, nikaamua kuandaa kitabu hiki ili watoto wapate uelewa wa mapema,” amesema.
Ameongeza kuwa kitabu hicho kimeandaliwa katika matoleo mawili Kiswahili na Kiingereza ili kukidhi mahitaji ya shule zinazotumia lugha tofauti za kufundishia.
“Elimu ya magonjwa yasiyoambukiza hususan saratani ni haba, hivyo tunahitaji juhudi za makusudi kuifikisha kwa jamii mapema,” amesema.
Naye mzazi Huya Issa amesema uzinduzi wa kitabu hicho ni hatua muhimu katika kuongeza uelewa wa afya kwa watoto na jamii.
“Nimefurahi sana kwa uzinduzi wa kitabu hiki, kitakuwa chachu ya maarifa kwa watoto wetu na jamii kuhusu magonjwa yasiyoambukiza. Niwatake wadau na walimu wakitumie vyema kueneza maarifa hayo,” amesema.
Uzinduzi huo unatajwa kuwa hatua muhimu ya kuanza kuingiza elimu ya afya katika ngazi za awali za elimu nchini.
Baraka Fundo ni mtaalamu wa fizikia tiba katika Taasisi ya Saratani Ocean Road, Dar es Salaam.
Kupitia kazi yake, amekuwa akihudumia wagonjwa wa saratani na kushuhudia changamoto za uelewa mdogo wa ugonjwa huo.
Uzoefu huo ulimsukuma kuandika Amani Rafiki Shujaa ili kusaidia kutoa elimu ya mapema kwa watoto na jamii kuhusu saratani na njia za kujikinga.
