Kichapo cha KMKM chaizidishia presha Mafunzo ZPL

MAFUNZO imeendelea kuwa na wakati mgumu katika msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar baada ya kukubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa KMKM.

Katika mechi hiyo ya mzunguko wa 22 iliyochezwa Aprili 10, 2026 kwenye Uwanja wa Mao A kisiwani Unguja, timu hizo ziliingia uwanjani zikitofautiana pointi mbili huku ushindi wa KMKM ukiifanya kufikisha pointi 32 ikikamata nafasi ya tisa, wakati Mafunzo ikisalia na pointi zake 27, nafasi ya 12.

Kwa mechi nane zilizobaki, Mafunzo ina kazi ya kuhakikisha haipotezi pointi ili kutoangukia kwenye mstari wa kushuka daraja kwani tofauti yake na timu inayofuatia katika hatari hiyo ambayo ni Polisi, ni pointi mbili pekee.

Katika mechi nane zilizobaki kwa Mafunzo, itacheza dhidi ya New King iliyopo nafasi ya kumi na pointi 29, Malindi (nafasi ya 14 pointi 24), Chipukizi (nafasi ya kumi pointi 28), Junguni (nafasi ya 15 pointi kumi), Kipanga (nafasi ya sita pointi 36), Muembe Makumbi (nafasi ya nane pointi 33) na Polisi (nafasi ya 13 pointi 25).

Awali timu hiyo ilikuwa ikinolewa na Kocha, Haji Nuhu ambaye aliondolewa kikosini hapo kwa kile kilichoelezwa kutokuwa na matokeo mazuri, nafasi yake ikachukuliwa na Salum Ali Haji.

Licha ya kufanya mabadiliko hayo, bado timu hiyo imeendelea kutokuwa na matokeo mazuri sana ambapo tangu kocha huyo achukue nafasi hiyo, ameshinda mechi moja kati ya sita, huku akitoa sare tatu na kupoteza mbili.

Matokeo ya Mafunzo chini ya kocha Salum ni; Mafunzo 1-1 Zimamoto, Polisi 1-1 Mafunzo, Mafunzo 0-0 JKU, Mafunzo 1-0 KMKM, KVZ 3-1 Mafunzo na KMKM 1-0 Mafunzo.

Katika mchezo mwingine wa ligi hiyo uliochezwa Aprili 10, 2026 kwenye Uwanja wa Mao B kisiwani Unguja, Kipanga imetoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya New King.