Dar es Salaam. Tanzania imechaguliwa kuwania vipengele 41 vya World Travel Awards 2026, hatua inayotajwa kuwa fursa kubwa ya kuitangaza nchi kimataifa na kuongeza ushindani wa sekta ya utalii.
Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) imesema uteuzi huo unaonesha namna vivutio vya Tanzania vinavyozidi kutambulika duniani na kuifanya nchi kuwa miongoni mwa vinara wa utalii barani Afrika na duniani.
Meneja Mawasiliano wa TTB, Pauline Mkama, akizungumza na waandishi wa habari leo Jumamosi, Aprili 11, 2026, amesema uteuzi huo unatokana na juhudi za pamoja za Serikali na sekta binafsi katika kuboresha huduma, kuhifadhi rasilimali za asili na kuendeleza kampeni za kuitangaza Tanzania nje ya nchi.
Amesema tuzo hizo si heshima tu, bali ni nafasi ya kuiweka Tanzania kwenye ramani ya dunia kama moja ya maeneo bora ya kutembelea.
“Wananchi na wadau wa utalii wanapaswa kushiriki kupiga kura kwa wingi ili kuhakikisha Tanzania inashinda katika vipengele vingi zaidi. Hii ni fursa ya kipekee ya kutangaza vivutio vyetu kwa dunia,” amesema Mkama.
Kwa mujibu wa TTB, baadhi ya vivutio vilivyopendekezwa ni pamoja na Amani Nature Forest, Mapango ya Amboni, Pugu Kazimzumbwi, Selous Game Reserve, Kilwa na maeneo mengine yenye urithi wa asili na kihistoria.
Pia, taasisi za serikali zikiwemo Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa) na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) zimewasilisha vivutio mbalimbali kuwania tuzo hizo.
“Ili kufanikisha ushindi huu, tumekuja na kampeni maalum ya ‘One Vote, One Click, One Destination.’ Mwisho wa upigaji kura ni Julai 17 mwaka huu,” amesema.
Takwimu za bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii mwaka 2025/2026 zinaonyesha kuendelea kuwapo kwa ongezeko la watalii, jambo linaloendelea kutengeneza soko la uhakika.
Idadi ya watalii wa kimataifa imeongezeka kutoka 922,692 mwaka 2021 hadi watalii milioni 2.141 mwaka 2024.
Idadi ya watalii wa ndani waliotembelea vivutio vya utalii imeongezeka kutoka 788,933 mwaka 2021 hadi kufikia watalii 3,218,352 mwaka 2024.
Hatua hii imewezesha idadi ya watalii kufikia milioni 5.360, sawa na asilimia 107.2 ya lengo la watalii milioni 5 kama ilivyoelekezwa kwenye Ilani ya CCM ya mwaka 2020.
