Dar es Salaam. Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu amesema Serikali imeanzisha mahusiano kwa lengo la kuunganisha Serikali na makundi mbalimbali ya kijamii, ikiwemo taasisi za dini.
Amesema lengo ni kuwaleta Watanzania pamoja kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya 2050 kwa upendo na amani.
Sangu ametoa kauli hiyo hivi karibuni wakati wa maadhimisho ya miaka 19 ya Kanisa la Neno la Upatanisho (The Reconciliation Church) yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Amesema azma ya Serikali katika jukumu jipya la ofisi hiyo ni kuunganisha makundi yote ya kijamii ikijumuisha taasisi za kidini, wadau wa siasa, taasisi zisizo za serikali na mashirika ya kiraia.
Katika hafla hiyo, Sangu amelishukuru kanisa hilo kwa mchango wao wa utoaji wa huduma na misaada mbalimbali kwa jamii zinazomzunguka kwa kuunga mkono jitihada za Serikali kwa kusaidia jamii zenye mahitaji na makundi maalumu.
“Serikali imeendelea kuona taasisi mbalimbali za kidini zikifanya kazi kubwa za kijamii, na ndani ya miaka 19 ya huduma za kanisa hili, bado tunashuhudia namna mnavyoiunga mkono Serikali kwa kufanya kazi kubwa, nasi tunathamini sana michango yenu mnayoitoa kwa jamii,“ amesema Sangu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kanisa hilo la WRC, Nabii Nicolaus Suguye ameishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kutambua mchango wa viongozi wa dini katika jamii kwa kuwaweka karibu, na kuwawezesha kufanya kazi pamoja.
Aidha, amepongeza hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali katika kuhakikisha amani, upendo, utulivu na mshikamano unaendelea kustawi nchini na kuwaleta pamoja watanzania wote bila kuangalia tofauti za dini na itikadi zao za kisiasa.
Pia, Nabii Suguye ametumia fursa hiyo kuiasa jamii kutoshiriki taarifa mbalimbali za uvumi katika mitandao ya kijamii zinazoweza kuleta taharuki na kuacha kufanya kazi zao za uzalishaji mali, huku akitolea mfano taarifa zilizosambaa zinazowahusisha wanaume kupoteza nyeti zao kwa kushikwa bega.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema makundi ya kidini na madhehebu mbalimbali, yamekuwa na mchango mkubwa katika kustawisha amani ya nchini, kutokana na mahubiri na mafundisho wanayoyatoa kwa waumini wao, sambamba na dua za kuliombea taifa wakati wote.
