Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi ametoa wito kwa vijana kusimama imara na kulinda umoja, kujenga uadilifu, kutumia elimu na ubunifu katika kukuza maendeleo ya nchi ili kuweza kumuenzi Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere kwa vitendo.
Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati akifungua Kongamano la Vijana katika Kumbukizi ya Miaka 104 ya Kuzaliwaa Baba wa Taifa, Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere, lililofanyika Ukumbi wa Chimwaga mkoani Dodoma, leo tarehe 11 Aprili 2026. Amesema ni muhimu kwa vijana kutambua wajibu wa msingi wa kizazi hiki, kwa kuhakakikisha wanafanya kila jitihada kuimarisha misingi ya kujitegemea kiuchumi, kiakili na kimaamuzi ili kuijenga nchi.
Makamu wa Rais amesema Hayati Baba wa Taifa alikuwa kiongozi aliyeunganisha Taifa na kutoa mchango mkubwa katika ukombozi wa Bara la Afrika. Amesema Taifa la Tanzania lilipata bahati ya pekee kuwa na Hayati Mwl. Nyerere kwa kuwa alichukia rushwa, ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka. Aliamini katika utu na uhuru wa mwanadamu ikiwemo msisitizo wa kuhakikisha kila wananchi anapata elimu.
Ameongeza kwamba Baba wa Taifa alitengeneza misingi ya amani, utulivu na mshikamano katika Taifa pamoja na kufundisha vitu vyote vinavyoweza kuleta mpasuko kama vile ukabila, dini, rangi, kupuuza maendeleo na usawa katika jamii.
Makamu wa Rais amesema ni dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuendeleza mshikamano na umoja ambao Baba wa Taifa aliujenga.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi wa Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwal. Nyerere ambaye ni Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Pinda ametoa rai kwa vijana kuhakikisha wanafanya jitihada za kujifunza historia ya Taifa ili kufahamu waliotoa mchango mkubwa katika historia hiyo.
Amewahimiza kusoma vitabu vilivyoandikwa kuhusu Hayati Mwal.Julius Kambarage Nyerere ili kufahamu mchango mkubwa aliyoutoa katika ukombozi wa Bara la Afrika na msisitizo alioutoa wa katika kuhakikisha umoja wa Afrika. Ameongeza Taasisi hiyo imejikita katika kutoa mchango kwa kuwasaidia viongozi vijana kuwa wazalendo na wanaowajibika.
Kongamano hilo limejadili mada mbalimbali zenye lengo la kuwajengea vijana uzalendo, uwajibikaji, matumizi sahihi ya mitandao na matumizi bora ya fursa zilizopo nchini.

.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)