YANGA imeijibu Simba kuhusu Mohamed Damaro anayeichezea kwa mkopo akitokea Singida Black Stars, huku rais wa klabu hiyo, Hersi Said akisema kuiingiza kwenye suala hilo ni kuikosea.
Leo Jumamosi, Hersi akiwa kwenye studio za TBC Taifa alizungumzia pia sakata la Damaro ambalo kwa sasa limeshika kasi kutokana na Simba kutaka kwenda Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi (CAS) kudai haki yao baada ya kutoridhishwa na majibu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Klabu ya Yanga inafuata taratibu zote za usajili, kuhusu mchezaji Damaro alisajiliwa akiwa mzawa baada ya kupata uraia Januari 2025 akiwa Singida Black Stars.
“Takribani mwaka mmoja na miezi kadhaa uliopita alikuwa amesajiliwa kama mchezaji wa Kitanzania na katika taratibu za kiusajili ni kwamba, ukishamsajili mchezaji unapata leseni inayokupa tafsiri ya kwamba mchezaji huyu ni mzawa au mgeni.
“Kwa hiyo leseni ya Damaro inasoma kama mzawa kutoka Januari 2025, sisi tukimtazama kwenye mifumo ambayo FIFA inaitambua anaonekana Mtanzania.
“Sisi tunapofanya programu zetu za kumtaka mchezaji tukiweka maanani kwamba wageni wanatakiwa 12, Damaro anasoma kama mzawa, wakati tunamuomba kutoka Singida alikuwa anasomeka hivyo, ukituingiza Yanga unatukosea.
“Amecheza nusu msimu kama mzawa na baada ya hapo usajili wa 2025-2026 akapata leseni mpya tena inayomtambua kama Mtanzania na ndiyo hiyo wakati tunamtoa Singida alikuwa anaitumia inayotolewa na mamlaka husika (TFF) na Uhamiaji pia unamtambua kama Mtanzania,” amesema Hersi.
Ikumbukwe kuwa, Aprili 2, 2026, TFF ilitangaza kutupilia mbali shauri lililokuwa limefikishwa mbele ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji kuhusu uhalali wa Damaro kuitumikia Yanga kama mchezaji mzawa.
Simba ilidai usajili wa Damaro mwenye asili ya Guinea kutua Yanga akitokea Singida Black Stars, umekiuka Kanuni ya 62(1) ya Ligi Kuu pamoja na Kanuni za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
Kamati katika uamuzi wake ilisema usajili hauna dosari kwa vile Damaro habanwi na kanuni zilizowasilishwa na Simba.
Kuhusu uwanja mpya, amesema: “Tumefika katika eneo zuri sana, sisi Yanga huwa tuna mikakati ambayo hairudi nyuma inayosema ‘Daima Mbele Nyuma Mwiko’, tulichokifanya tulitangaza tenda na GSM ikashinda.
“Baada ya hapo tukakaa nao na wakaleta mchoro wa kwanza na tukatoa maoni yetu na jana (juzi Ijumaa) walikamilisha michoro pamoja na gharama za ujenzi pia, hivyo kilichobaki ni sisi kukaa na GSM kuona tunaone ni kwa kiasi gani uwanja utakuwa na gharama ili tufanye makubaliano.
“Hatua tuliyonayo tunaenda kukutana na kukubaliana umoja kati ya GSM na Yanga hususani katika mradi huu wa uwanja. Baada ya hapo tukishatangaza na michoro iko tayari atapatikana mkandarasi na ujenzi utaanza,” amesema Hersi
