POLISI YAKANUSHA UHALIFU WA KUTUMIA ANUANI NA WATOTO

******

Jeshi la Polisi nchini Tanzania limewataka wananchi kupuuza taarifa na ujumbe unaoendelea kusambazwa kwenye Mitandao mbalimbali ya Kijamii ikidai kuwa kuna watoto katika Mitaa mbalimbali nchini wenye karatasi za kuonesha anuani zao, wakieleza kuwa wamepotea na kwamba ukimpeleka mtoto huyo kwenye anuani husika unajipeleka kwa wahalifu.

“Ujumbe huu ni uzushi na uongo wenye kutaka kuleta taharuki na hofu kwa wananchi, Jeshi la polisi linatoa wito kwa umma kuupuuzia na kuacha kuendelea kusambaza kwani kufanya hivyo unatenda kosa la jinai kwa mujibu wa sheria ya makosa ya kimtandao ya mwaka 2015.” Amesema Msemaji wa Jeshi la Polisi, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) David Misime leo Jumamosi Aprili 11, 2026 katika taarifa yake kwa Vyombo vya habari.