Yanga yamuita mezani kiungo Mghana

MWANASPOTI lina taarifa kwamba, kuna kitu kinaendelea kwa siri baina ya kiungo mkabaji wa Azam FC, Mghana James Akaminko na Yanga kinachohusu usajili kuelekea msimu wa 2026-2027.

Ikiwa imebaki miezi miwili kabla ya msimu huu kumalizika, Mwanaspoti limepata taarifa za ndani zinazosema kuna mazungumzo yanayoendelea kwa kiungo huyo na uongozi wa Yanga, lakini pia waajiri wake wa sasa kwa maana ya Azam nao wamemuita mezani kufanya mazungumzo ya mkataba mpya.

Kiungo huyo anayetumia mguu wa kulia, aliyezaliwa Septemba 16, 1995 (umri wa miaka 30) nchini Ghana, alijiunga na Azam Julai 14, 2022, kwa sasa amebakiza miezi miwili mkataba wake kumalizika huku kanuni zikimruhusu kufanya mazungumzo na klabu nyingine zinazomuhitaji.

Chanzo kutoka ndani ya Yanga kimeliambia Mwanaspoti kuwa mchakato wa kumpata kiungo huyo ulianza tangu dirisha dogo la Januari 2026 ambapo viongozi wa klabu hiyo walikutana na Akaminko huko Zanzibar wakati wa mashindano ya Kombe la Muungano 2026 wakafanya mazungumzo ya awali.

“Mpango wa Yanga ni kumsajili katika dirisha kubwa baada ya kumaliza mkataba wake,” kilisema chanzo hicho na kuongeza.

“Unajua Akaminko na viongozi wa Yanga walikutana Zanzibar katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi, hapo ndipo mazungumzo yalipoanza kipindi ambacho alibakisha miezi sita kwenye mkataba wake na sasa wanaendelea vizuri, wapo hatua za mwisho.

“Hata hivyo, tumesikia Azam wamemuita mezani kwa ajili ya kumuongezea mkataba baada ya kuona kuna klabu zingine zimeanza kumfuatilia kiungo huyo ambaye ni kama ameamua kuchagua kuondoka baada ya kukaa hapo kwa takribani miaka minne.”

Endapo hilo likifanikiwa, Akaminko atakwenda kukutana na ushindani wa Duke Abuya, Aziz Andabwile na Mohamed Damaro aliyejiunga na klabu hiyo akitokea Singida Black Stars.

Akaminko katika mechi sita za hivi karibuni, tano alizocheza kwa dakika 90 kila moja dhidi Simba, Singida Black Stars, Yanga, Dodoma Jiji na Mbeya City, alicheza kwa kiwango cha juu, huku akiikosa mechi ya Mashujaa.

Katika mechi hizo ameonyesha kutengeneza pacha nzuri na kiungo mwenzake wa kati, Himid Mao licha ya ulinzi pia wanasaidia kutuliza timu, kucheza kwa utulivu wa kusaka matokeo ya ushindi.

Kiungo huyo mechi hizo alizocheza matokeo yalikuwa Dodoma Jiji 0-3 Azam, Azam 0-0 Yanga, Azam 0-0 Simba, Singida Black Stars 1-1 Azam na Mbeya City 0-0 Azam.

Mwanzoni mwa msimu huu, Akaminko ilionekana nafasi yake ya kucheza ndani ya Azam ni finyu akishindania namba na Yahya Zayd, Adolf Mtasingwa, Himid Mao na Sadio Kanoute, lakini tangu timu hiyo ishiriki Kombe la Mapinduzi 2026, kiungo huyo amepindua meza na kurejea kuwa mchezaji muhimu.

Tangu Kombe la Mapinduzi 2026, Akaminko amekuwa akifanya vizuri wakati huu ambao viungo wengine wa ukabaji wakisumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara ambao ni Zayd na Mtasingwa.

Endapo makubaliano ya Yanga na Akaminko yatafikia pazuri kiungo huyo msimu ujao atatua mitaa ya Jangwani kwenda kuongeza nguvu ndani ya kikosi hicho ambacho pia kitalazimika kupunguza mchezaji mmoja wa kimataifa ili aingie Mghana huyo.