Kilio cha Chadema, ACT Wazalendo kwa Dk Chakwera

Dar es Salaam. Vyama vya upinzani nchini, Chadema na ACT Wazalendo, vimewasilisha malalamiko yao kwa Mjumbe Maalumu wa Jumuiya ya Madola, Dk Lazarus Chakwera, kuhusu haki za binadamu na mwenendo wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, kabla na baada yake.

Katikati ya malalamiko hayo, Chadema kimewasilisha ombi rasmi kwa Dk Chakwera, ambaye ni Rais wa zamani wa Malawi, la kuruhusiwa kwenda kumuona Tundu Lissu (Mwenyekiti wa Chadema), aliyepo gerezani akikabiliwa na shtaka la uhaini.

Wakati vyama hivyo vikieleza malalamiko hayo, Serikali kwa upande wake imemweleza Dk Chakwera hatua mbalimbali inazozichukua kuhakikisha nchi inaendelea kuwa tulivu, huku demokrasia na amani vikitawala.

Dk Chakwera yupo nchini kwa ziara ya kikazi baada ya kuteuliwa na Jumuiya ya Madola, ambapo anafanya mazungumzo na viongozi wa Serikali, wadau wa siasa na asasi za kiraia ili kujenga mshikamano na hatua za maridhiano.

Ujio wa Dk Chakwera umekuja baada ya kupita mwezi mmoja tangu Tanzania ipokee ujumbe mwingine wa Jumuiya ya kimataifa, Parfait Onanga-Anyanga, ambaye ni Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), aliyefanya ziara nchini kuanzia Machi 8 hadi 12.

ACT Wazalendo ndicho kilikuwa chama cha kwanza kuonana na Dk Chakwera na kumpa mambo manne, ikiwemo madai kuwa Uchaguzi Mkuu wa Tanzania wa Oktoba 29, 2025 haukuwa huru na wa haki.

Chama hicho kikuu cha upinzani Zanzibari kilidai uchaguzi huo ulikuwa na ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi, na kwamba kulikuwepo na matumizi ya nguvu kupita kiasi.

Madai mengine yaliyowasilishwa na ACT Wazalendo kupitia kiongozi wa chama hicho, Dorothy Semu, ni ukiukwaji wa haki za binadamu kabla na baada ya uchaguzi, kuminywa kwa uhuru wa haki za kiraia na kijamii, pamoja na hitaji la mageuzi ya kisiasa na uwajibikaji.

Katika taarifa yake kwa umma iliyotolewa na Semu, ACT Wazalendo imedai kuwa uchaguzi huo “uligeuzwa kuwa mchakato wa kupanga matokeo,” na kwamba matukio yaliyofuata yalileta mgogoro wa uhalali wa kisiasa wa Serikali inayoongozwa na Samia Suluhu Hassan.

Chama hicho kimesema tathmini yake inategemea ushahidi uliokusanywa kabla, wakati na baada ya uchaguzi, ikiwemo hatua za uteuzi wa wagombea, upigaji kura, uhesabuji na utangazaji wa matokeo.

“Kwa mujibu wa tathmini yetu, Tanzania kwa sasa inakabiliwa na hali mbaya ya kisiasa inayoashiria kuporomoka kwa demokrasia ya vyama vingi na kuimarika kwa utawala unaotegemea vyombo vya usalama,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha, ACT Wazalendo pia imedai wagombea wake wa urais na ubunge waliondolewa katika mazingira yasiyo ya haki, huku zaidi ya asilimia 30 ya wagombea wa ubunge na asilimia 22 ya udiwani wakikosa nafasi ya kushiriki.

Kuhusu uminywaji wa uhuru na haki za kijamii, taarifa hiyo imeeleza hali hiyo imejidhihirisha kupitia vikwazo katika uhuru wa kujieleza, kukusanyika na kushirikiana, sambamba na ongezeko la hofu miongoni mwa jamii, hali inayoathiri ushiriki wa wananchi katika masuala ya kijamii na kisiasa.

Kuhusu mageuzi ya kisiasa na uwajibikaji unaohitajika, ACT Wazalendo imesema hali ya sasa inaashiria kudhoofika kwa demokrasia na kupungua kwa uhuru wa kiraia na kijamii.

Chadema kiliwasilisha taarifa ya matukio ya kabla na baada ya Oktoba 29, 2025, ikiwemo madai ya kukamatwa kwa viongozi wake, akiwemo Tundu Lissu, pamoja na tuhuma za utekaji, huku kikimuomba Dk Chakwera kuruhusiwa kumtembelea Lissu gerezani, ambaye ametimiza mwaka mmoja tangu awe kizuizini.

Taarifa kwa umma ya Chadema ilieleza kuwa ujumbe wa chama hicho uliokwenda kuonana na Dk Chakwera uliongozwa na viongozi waandamizi, akiwemo John Heche (Makamu Mwenyekiti Bara).

Katika taarifa hiyo, imeelezwa kuwa Dk Chakwera alipokea msimamo wa Kamati Kuu ya Chadema na kupewa maelezo ya kina kuhusu matukio yaliyotokea kabla na baada ya Oktoba 29, 2025, ikiwemo mauaji ya raia na kuzuiwa kwa shughuli za kisiasa.

Miongoni mwa msimamo wa Kamati Kuu ya Chadema ni kutokubaliana na matokeo ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, kutaka Katiba Mpya, Tume Huru ya Uchaguzi, mageuzi ya mfumo wa uchaguzi, pamoja na uchunguzi huru kuhusu matukio ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Kwa mujibu wa taarifa ya Chadema, Dk Chakwera amepokea taarifa hizo na kuelezwa kwa kina kuhusu mazingira ya kisiasa nchini, huku ujumbe wake ukiendelea kukusanya taarifa kuhusu tuhuma za ukiukwaji wa haki za binadamu.

Dk Chakwera aliwasili Aprili 8, 2026 na alianza ratiba yake kwa kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, Aprili 9, 2026 jijini Dar es Salaam. Mkutano huo ulilenga kumkaribisha nchini na kuanza majukumu yake.

Aidha, Dk Chakwera amekutana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Profesa Palamahamba Kabudi, ambaye aliongoza ujumbe wa Tanzania.

Profesa Kabudi alimweleza Dk Chakwera hatua mbalimbali ambazo Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inachukua kuhakikisha inaimarisha demokrasia na amani nchini ili kudumisha umoja wa kitaifa.

“…tumemweleza mambo mengi kuhusu Tanzania na historia ya nchi hii tangu ipate Uhuru mwaka 1961, hali ya siasa na demokrasia nchini, na hatua ambazo Serikali inaendelea kuchukua ili kuhakikisha nchi inaendelea kuwa tulivu, hivyo kuwezesha Watanzania kushiriki kikamilifu katika kujenga uchumi jumuishi,” alisema Profesa Kabudi.

Pia, Dk Chakwera amekutana na kufanya mazungumzo na watendaji wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, wakiongozwa na Jaji Francis Mutungi (Msajili wa Vyama vya Siasa).