Safari ya kihistoria ya Artemis II haikuwategemea tu teknolojia ya hali ya juu, bali pia uwezo, taaluma na uzoefu wa wanaanga wanne waliounda timu yake.
Wakiwa wamechaguliwa na NASA kwa vigezo vikali, kila mmoja wao ana historia ya kipekee ya elimu na kazi iliyowaandaa kwa safari hiyo ya kipekee kuelekea Mwezi na kurudi.

Reid Wiseman – Kiongozi Mwenye Uzoefu wa Kijeshi na Teknolojia
Kamanda wa misheni, Reid Wiseman, ni rubani wa zamani wa jeshi la majini la Marekani aliyejikita katika uhandisi wa mifumo ya kompyuta.
Akiwa na shahada ya Computer Systems Engineering, Wiseman ameunganisha taaluma ya teknolojia na uzoefu wa kijeshi, jambo lililomuwezesha kuongoza misheni kwa ustadi mkubwa. Kabla ya Artemis II, tayari alikuwa na uzoefu wa safari za anga kupitia Kituo cha Kimataifa cha Anga (ISS), hali iliyompa uwezo wa kukabiliana na changamoto za anga za mbali.

Victor Glover – Rubani na Mhandisi wa Kiwango cha Juu
Rubani wa misheni hiyo, Victor Glover, ni mmoja wa wanaanga waliobobea zaidi katika uendeshaji wa ndege na mifumo ya anga. Akiwa na elimu ya juu katika Uhandisi (Engineering) pamoja na shahada za uzamili katika Flight Test Engineering na Military Science, Glover ameonesha umahiri katika majaribio ya ndege na safari za anga.
Uzoefu wake kama mwanaanga wa ISS ulimuweka katika nafasi nzuri ya kushiriki safari hii ya kihistoria.

Christina Koch – Mwanamke Aliyevunja Rekodi Angani
Kwa upande wa Christina Koch, yeye ni mhandisi wa umeme na mwanafizikia aliyebobea katika tafiti za mazingira magumu.
Akiwa na shahada katika Electrical Engineering na Physics, Koch alijizolea umaarufu kwa kuvunja rekodi ya kukaa muda mrefu zaidi angani kwa mwanamke.
Uzoefu wake katika tafiti za kisayansi ulimfanya kuwa mhimili muhimu katika misheni ya Artemis II, hasa katika utafiti wa mabadiliko ya mwili wa binadamu angani.


Jeremy Hansen – Mwakilishi wa Canada Mwenye Utaalamu wa Anga
Mwanaanga kutoka Canadian Space Agency, Jeremy Hansen, aliongeza sura ya kimataifa katika misheni hiyo. Akiwa na shahada ya Uhandisi wa Anga (Space Engineering), Hansen pia ni rubani wa jeshi la anga la Canada.
Uwezo wake katika mifumo ya anga na uzoefu wa kijeshi ulimuwezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kisayansi na kiufundi za misheni.

Kwa pamoja, wanaanga hawa wanne wanaonesha jinsi elimu ya juu, uzoefu wa vitendo na maandalizi ya muda mrefu vinavyoweza kumuwezesha binadamu kufikia malengo makubwa kama safari ya Mwezi. Misheni ya Artemis II si tu mafanikio ya teknolojia, bali pia ni ushahidi wa uwekezaji katika elimu na utaalamu wa hali ya juu unaoendelea kuisukuma dunia mbele katika uchunguzi wa anga.