Simu zikizidi, malezi yanayeyuka kimyakimya

Dar es Salaam. Katika ulimwengu wa leo unaokimbizana na muda, wazazi wengi hasa kinamama wamejikuta wakibadili mtindo wa malezi bila hata kutambua.

Shughuli za kiuchumi, utafutaji na presha za maisha zimewafanya baadhi yao kuwa mbali kimwili na watoto wao, lakini karibu kwa njia ya simu.

Sauti ya mama imebaki kusikika mara kwa mara ikiuliza kwa njia ya simu; “Dada, wamekula?” wengine utasikia wakiuliza; “wamerudi salama kutoka shuleni, wanafanya nini muda huu.”

Maswali yote hayo yanaashiria kujali, lakini ukijiuliza kwa kina, ni wazi kuwa maswali haya ya wazazi au mzazi yanaacha pengo kubwa lisiloonekana baina yake na watoto wao.

Kwa nje, inaweza kuonekana kama mama anatimiza wajibu wake kikamilifu. Lakini ndani yake, kuna upungufu wa msingi wa malezi unaojengwa polepole.

Tunaambiwa na wataalamu kwamba malezi si taarifa, ni uwepo. Ni kugusa maisha ya mtoto kwa karibu, si kusimamia kutoka mbali.

Mtoto anayelelewa kwa mfumo huu wa ‘malezi ya simu’ hukosa kitu muhimu sana ambacho nacho ni uwepo halisi wa mzazi. Uwepo huu si wa kumwona tu mzazi, bali ni wa kujenga hisia ya kuonekana, kusikilizwa na kuthaminiwa.

Mtoto anapokua akizoea kwamba mama yake yupo kwa sauti tu, si kwa matendo, huanza kujenga pengo la kihisia.

Anaweza kuanza kujitenga, kuwa na ukimya usioeleweka au hata kutafuta upendo na uangalizi nje ya familia yake.

Zaidi ya hapo, tunaambiwa kuwa mawasiliano ya simu yana mipaka mikubwa. Simu haisemi kila kitu. Haiwezi kufichua macho ya mtoto yaliyochoka, huzuni iliyofichika au mabadiliko madogo ya tabia yanayoweza kuwa ishara ya tatizo kubwa. Mtoto anaweza kusema niko sawa, lakini uso wake ukaonyesha tofauti kabisa.

Haya ni mambo ambayo mzazi wa mbali hawezi kuyaona na hivyo kupoteza nafasi ya kuchukua hatua mapema.

Hali hii pia huleta mabadiliko ya kimamlaka ndani ya familia. Pale ambapo dada wa kazi anakuwa ndiye anayekaa muda mwingi na watoto, taratibu anaanza kuchukua nafasi ya mzazi katika macho ya mtoto.

Anakuwa msikilizaji, mlezi na wakati mwingine mtoa uamuzi wa kila siku. Mtoto anaanza kumtambua zaidi yeye kuliko mama yake.

Hii inaweza kuathiri nidhamu, heshima na hata utii, kwa sababu mamlaka ya mzazi halisi hupungua kadiri anavyoonekana kuwa wa mbali.

Pia, kuna hatari ya taarifa kupotoshwa au kupunguzwa. Si mara zote dada wa kazi ataelezea kila kitu kwa usahihi au kwa kina kinachohitajika.

Wakati mwingine kwa hofu, uzembe au kutoona umuhimu, dada anaweza kuacha kumweleza mtoto baadhi ya mambo.

Hivyo hii humfanya mzazi kufanya uamuzi kwa msingi wa taarifa pungufu, hali inayoweza kuathiri vibaya ustawi wa mtoto.

Na mzazi anapaswa kutambua kuwa athari hizo hazionekani mara moja. Ni kama mmomonyoko wa polepole unaoanza chini ya ardhi.

Lakini baada ya muda, matokeo yake hujitokeza wazi, mtoto asiye na ukaribu na mzazi, mara nyingi hukumbwa na changamoto za kihisia, au anashindwa kuwa na mwelekeo thabiti wa maadili.

Hivyo, swali la msingi linabaki kuwa mzazi afanye nini katika hali kama hii?

Inaelezwa kwamba, ni lazima mzazi arejeshe thamani ya uwepo wake. Hata kama ratiba ni ngumu, anapaswa kutenga muda maalum wa kuwa na watoto wake ana kwa ana.

Si lazima uwe na muda mrefu, bali hata mfupi tu wa kuzungumza, kusikiliza, kucheka na hata kushirikiana na wanao katika mambo madogo ya kila siku. Hapo ndipo uhusiano wa kweli hujengwa ndivyo tunavyoambiwa na wataalamu wa malezi.

Lakini pia tukumbuke kuwa mzazi anapaswa kujihusisha moja kwa moja katika maisha ya mtoto wake. Anapaswa kujua anashirikiana na marafiki wa aina gani sambamba na maendeleo yake shuleni lengo ni kutaka kujua ni changamoto zipi anazokutana nazo badala ya kumuachie dada aje akusimulie.

Ushiriki huu mara nyingi unampa mtoto hisia ya kuthaminiwa na hujenga ujasiri wa kufunguka kwa mzazi wake.

Ni vizuri simu ibaki kuwa chombo cha nyongeza, si mbadala wa malezi. Ni vizuri kupiga simu kujua hali ya mtoto, lakini isichukue nafasi ya macho, masikio na moyo wa mzazi.

Ingawa dada wa kazi ni msaada muhimu katika familia, hapaswi kuchukua nafasi ya mzazi. Uamuzi malezi ya msingi yanapaswa kubaki mikononi mwa mzazi mwenyewe hususan mama.

Nasema hivyo kwa sababu malezi yanahitaji uwekezaji wa muda, hisia na uwepo. Hakuna teknolojia inayoweza kuchukua nafasi ya mzazi katika maisha ya mtoto.

Sauti ya simu inaweza kufika, lakini haiwezi kubeba joto la upendo, mguso wa faraja, au macho yanayoona zaidi ya maneno.

Ikiwa tunataka kulea kizazi chenye afya ya akili, maadili na mwelekeo sahihi, basi ni lazima tukubali ukweli kwamba watoto hawahitaji simu zetu zaidi, wanatuhitaji sisi wazazi.