Dar es Salaam. Katika kipindi ambacho ndoa nyingi zinavunjika kwa kasi isiyokuwa ya kawaida, swali moja muhimu linapaswa kuulizwa kwa dhati: tunawaandaa vipi wataalamu wa kusaidia wanandoa?
Jamii imekuwa ikishuhudia migogoro ya ndoa inayotokana na sababu ndogo zinazogeuka kuwa kubwa kwa kukosa ushauri sahihi.
Watu wanaoa wakiwa na elimu ya taaluma mbalimbali, lakini bila elimu ya ndoa. Wengine wanaingia kwenye ndoa wakiwa wamebeba majeraha ya kihisia, mitazamo potofu na matarajio yasiyo halisi.
Katika mazingira haya, hitaji la washauri wa ndoa waliobobea si hiari tena, bali ni la lazima. Ndiyo maana vyuo vinapaswa kupika washauri wa ndoa kwa makusudi, kwa kuanzisha na kuimarisha kozi maalum hasa kwa wanaosomea saikolojia.
Ndoa ni taasisi nyeti inayogusa hisia, akili, mwili, maadili na jamii kwa ujumla. Si jambo la kushughulikiwa kwa kubahatisha au kwa uzoefu wa mtu binafsi pekee.
Hata hivyo, katika jamii zetu, ushauri wa ndoa bado unaendeshwa zaidi kwa mazoea, imani binafsi au uzoefu wa maisha, bila misingi thabiti ya kitaaluma. Hili ndilo pengo ambalo vyuo vikuu vinapaswa kulijaza.
Mwanafalsafa Sigmund Freud anasema: “Migogoro mingi ya maisha ya watu wazima huanzia katika maeneo ambayo hayakushughulikiwa vizuri kihisia.” Kauli hii inaonesha wazi kuwa matatizo ya ndoa mara nyingi si ya sasa tu, bali ni mizizi ya historia ya mtu kisaikolojia. Hivyo, mshauri wa ndoa anapaswa kuwa na elimu ya kina ya saikolojia ya binadamu, si nasaha za juu juu.
Kwa nini kozi hizi muhimu?
Kwa sasa, wanafunzi wengi wa saikolojia husoma kwa upana masuala ya tabia, afya ya akili, ushauri nasaha kwa ujumla na saikolojia ya jamii.
Hata hivyo, ndoa kama eneo mahsusi la maisha ya binadamu mara nyingi halitiliwi mkazo unaostahili. Ndoa huachwa kama mada ndogo ndani ya kozi pana, hali inayosababisha wahitimu wengi kukosa ujuzi wa kina wa kushughulikia changamoto za wanandoa.
Kuanzishwa kwa kozi maalum za ushauri wa ndoa kutasaidia kutoa wataalamu waliobobea katika kuelewa mienendo ya uhusiano wa kimapenzi, migogoro ya wanandoa, mawasiliano ndani ya ndoa, masuala ya jinsia, uzazi, malezi, usaliti, msongo wa mawazo na mabadiliko ya kihisia ndani ya ndoa. Haya ni masuala yanayohitaji mbinu maalum za kitaaluma, si busara za jumla.
Mwandishi na mwanasaikolojia, Carl Jung anasema kukutana kwa watu wawili ni kama kukutana kwa dunia mbili. Kauli hii inaakisi ugumu wa ndoa. Kila mmoja huja na historia yake, majeraha yake, ndoto zake na hofu zake. Bila mshauri aliyeandaliwa vizuri, dunia hizi mbili zinaweza kugongana na kusababisha maumivu makubwa.
Kozi maalum zitawasaidia wanafunzi kuelewa kuwa ndoa si tu mapenzi, bali ni mfumo unaohitaji ujuzi wa mawasiliano, udhibiti wa hisia na utatuzi wa migogoro. Hii itasaidia pia kuondoa dhana potofu kwamba mtu yeyote mzoefu wa maisha anaweza kuwa mshauri wa ndoa. Uzoefu ni muhimu, lakini bila elimu, unaweza kuwa hatari.
Umuhimu wa washauri wa ndoa
Ndoa inapovunjika, athari zake haziishii kwa wanandoa pekee. Watoto huumia, familia pana huathirika, na jamii hupoteza uthabiti. Hivyo, mshauri wa ndoa si msaidizi wa watu wawili tu, bali ni mlinzi wa ustawi wa jamii kwa ujumla. Kadiri ndoa zinavyoimarika, ndivyo jamii inavyokuwa imara.
Chinua Achebe, aliwahi kuandika: ‘’Jamii huanguka pale familia inaposhindwa kusimama.” Kauli hii inatoa uzito wa hoja kuwa kuwekeza katika ushauri wa ndoa ni kuwekeza katika mustakabali wa jamii. Vyuo vikitoa washauri waliobobea, vitakuwa vimechangia moja kwa moja katika kuimarisha familia.
Washauri wa ndoa waliopikwa vyuoni watakuwa na uwezo wa kusaidia kabla ndoa haijavunjika. Ushauri wa kabla ya ndoa, kwa mfano, ni eneo linalopuuzwa sana. Watu wengi huoa wakiwa hawajielewi, hawajui namna ya kushughulikia migogoro, wala hawajui matarajio yao halisi.
Mshauri aliyesomea kwa kina ataweza kuwasaidia wanandoa watarajiwa kujitathmini, kujifunza mawasiliano na kuweka msingi imara wa ndoa yao.
Mwandishi na mtaalamu wa masuala ya uhusiano, Erich Fromm, anasema: “Kupenda ni sanaa inayohitaji maarifa na juhudi.” Ndoa ni sehemu ya sanaa hiyo ya kupenda. Bila maarifa, mapenzi huchoka. Bila juhudi, ndoa hufa. Washauri wa ndoa waliobobea watasaidia kufundisha sanaa hii kwa vitendo.
Zaidi ya hayo, katika dunia ya sasa inayokumbwa na mabadiliko ya kasi ya kijamii, ndoa zinakutana na changamoto mpya: mitandao ya kijamii, mabadiliko ya majukumu ya kijinsia, shinikizo la kiuchumi na mabadiliko ya matarajio ya maisha.
Changamoto hizi zinahitaji washauri wanaoelewa muktadha wa sasa, si wale wanaotegemea misingi ya zamani pekee. Vyuo vina nafasi ya kuandaa washauri wanaoendana na wakati.
Vyuo vikuu vina wajibu mkubwa wa kuandaa rasilimali watu kwa ajili ya jamii. Kama kuna uhaba wa washauri wa ndoa waliobobea, basi ni ishara kuwa mfumo wa elimu una pengo.
Kuanzishwa kwa kozi maalum za ushauri wa ndoa ndani ya saikolojia kutahitaji mitalaa inayolenga vitendo, mafunzo ya vitendo na utafiti unaohusiana moja kwa moja na ndoa katika muktadha wa Kiafrika.
Mwandishi na mwanazuoni wa elimu, Paulo Freire, aliwahi kusema elimu isipojibu mahitaji ya jamii, basi imekosa dhamira yake.” Kauli hii inapaswa kuwashtua watunga sera za elimu. Jamii inalia kwa ndoa zinazovunjika, watoto wanaolelewa bila utulivu wa kifamilia, na msongo wa mawazo unaoongezeka. Elimu ya juu haina budi kujibu kilio hiki.
Serikali na vyuo vinapaswa kushirikiana kuanzisha programu rasmi za ushauri wa ndoa, kutoa ithibati kwa wataalamu hawa, na kuweka viwango vya kitaaluma. Hii itasaidia kuondoa ushauri holela unaoweza kuharibu zaidi ndoa badala ya kuziokoa.
Aidha, itatoa heshima na hadhi kwa taaluma ya ushauri wa ndoa kama ilivyo kwa taaluma nyingine za afya ya akili.
Kwa upande wa wanafunzi wa saikolojia, kuwepo kwa kozi hizi kutawapa fursa ya kujikita katika eneo lenye mahitaji makubwa ya ajira na huduma. Wataweza kufanya kazi katika hospitali, vituo vya ushauri, taasisi za dini, mashirika ya kijamii na hata kujiajiri. Hii ni fursa ya kitaaluma na kijamii kwa wakati mmoja.
Kwa ujumla, mustakabali wa ndoa zetu hauwezi kuachwa mikononi mwa bahati au mazoea. Unahitaji wataalamu waliopikwa kwa makusudi maalumu.
