Coastal Union yarudi kwa Fikiri Elias, amwaga ahadi nzito

ALIYEKUWA Kocha wa KenGold ya mkoani Mbeya, Fikiri Elias amefikia makubaliano ya kujiunga na kikosi cha Coastal Union hadi mwishoni mwa msimu huu akichukua nafasi ya Mohamed Muya, aliyeondoka Aprili 8, 2026 kutokana na mwenendo mbaya.

Awali, Fikiri alihusishwa kujiunga na Mashujaa kwa ajili ya kurithi mikoba ya Kocha Salum Mayanga, aliyeondoka ndani ya kikosi hicho, Februari 3, 2026, ingawa dili hilo halikufanikiwa na badala yake Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ akapewa mikoba hiyo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Fikiri amesema ni kweli amefikia makubaliano ya kukiongoza kikosi hicho baada ya kukaa nje kwa muda mrefu, japo ni mapema kuzungumza chochote kwa sasa kwa sababu ndio kwanza amekutana na wachezaji wa timu hiyo.

“Natambua kiu ya mashabiki na viongozi wa Coastal Union kwa sababu nimeshawahi kufanya kazi hapa, ili tufikie malengo ya pamoja ni lazima ushirikiano uwepo kati yetu, naamini hakuna kitakachoharibika kwa mechi zilizobaki,” amesema Fikiri.

Kocha huyo alikuwa hana timu ya kuifundisha tangu alipoachana na KenGold Septemba 17, 2024, kwa makubaliano ya pande mbili, baada ya mwenendo mbaya katika Ligi Kuu jambo lililosababisha kushuka daraja na kucheza Ligi ya Championship msimu huu.

Msimu wa 2024-2025, Fikiri aliiongoza KenGold katika mechi tatu za Ligi Kuu Bara na kupoteza zote, akichapwa mabao 3-1 dhidi ya Singida Black Stars, Agosti 18, 2024, (2-1) dhidi ya Fountain Gate, Septemba 11, 2024 na 1-0 mbele ya KMC, Septemba 16, 2024.

Fikiri anakuwa kocha wa tatu msimu huu kuifundisha Coastal Union, baada ya awali kikosi hicho kuanza na Alli Mohammed Ameir, aliyeondoka Oktoba 1, 2025, kisha kuteuliwa Muya, Oktoba 6, 2025, kisha kuondoka Aprili 8, 2026.

Kwa siku 184, Muya aliiongoza Coastal katika mechi 15 za Ligi Kuu Bara msimu wa 2025-2026, ambapo alishinda mbili, sare saba na kuchapwa sita, huku kikosi hicho kikifunga mabao 11 na kuruhusu 17, akikiacha nafasi ya 13 kwenye msimamo na pointi 16.

Hadi Muya anaondoka, Coastal Union ilikuwa imecheza jumla ya mechi 18 za Ligi Kuu Bara msimu huu, ikishinda tatu, sare saba na kupoteza nane, ikifunga mabao 13 na kuruhusu 21.