Arusha. Wanafunzi wasichana wenye ulemavu wa kusikia wanakabiliwa na changamoto mbalimbali wakati wa ukuaji, ikiwemo kukosa taarifa sahihi kuhusu hedhi na afya ya uzazi, ukosefu wa mawasiliano kati yao na jamii ikiwemo wazazi pamoja na upungufu wa vifaa salama vya kujikinga wakati wa hedhi.
Mwalimu wa wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia na mlezi wao, Veila Mkenda, amesema hayo jana, Jumamosi Aprili 11, 2026, wakati wa uzinduzi wa mradi wa mafunzo ya afya ya uzazi na hedhi salama kwa wasichana wenye ulemavu wa kusikia jijini Arusha.
Amesema kwa uzoefu wake wa zaidi ya miaka 10, changamoto kubwa ni kushindwa kuwasiliana kati ya watoto hao na wazazi au walezi wao, hasa wanapofikia balehe, kutokana na jamii kutojua lugha ya alama.
Ameongeza kuwa hali hiyo huwafanya watoto hao kukosa msaada wanapopata hedhi kwa mara ya kwanza, hali inayowasababishia hofu na mkanganyiko.
“Inapotokea hedhi, wanajiuliza nini kimetokea. Shuleni tunafuata mtaala uliopo, lakini baadhi yao hujiondoa darasani au kushindwa kuhudhuria masomo,” amesema.
Mkenda ameeleza kuwa aliwahi kubaini changamoto hiyo kupitia mwanafunzi aliyekuwa akiomba ruhusa mara kwa mara kwenda chooni na kujificha kwa muda mrefu.
“Nilipomfuata, ndipo akaniambia amepata damu kumbe ni hedhi. Alijaribu kumweleza mzazi wake lakini hawakuelewana kwa sababu hakujua lugha ya alama,” amesema.
Ameongeza kuwa wengi wao hukosa vifaa sahihi vya kujikinga na hulazimika kutumia vitambaa au tishu kutokana na ukosefu wa elimu na rasilimali.
Akisaidiwa kutafsiriwa, mwanafunzi wa darasa la saba, Glory Bilasho, amesema wao hukumbana na changamoto kubwa kutokana na wazazi na jamii kutojua lugha ya alama.
“Nilipopata hedhi kwa mara ya kwanza nilidhani ni jambo la ajabu. Nilijaribu kumweleza mzazi wangu lakini hatukuelewana. Nilijificha sana hadi nilipopata elimu,” amesema.
Kutokana na changamoto hizo, Shirika lisilo la kiserikali la Msichana Imara Foundation, kwa kushirikiana na Itel Tanzania, wamezindua mradi wa mwaka mmoja wa kutoa mafunzo ya afya ya uzazi na hedhi salama kwa wasichana 300 kutoka jijini Arusha.
Ofisa Miradi wa shirika hilo, Naishorwak Emanuel, amesema unalenga kuwapatia wasichana hao elimu sahihi pamoja na vifaa vya kujikinga wakati wa hedhi.
Amesema mafunzo yatatolewa kwa kutumia lugha ya alama na yatahusisha mada mbalimbali ikiwemo ukuaji na balehe, mabadiliko ya mwili na hisia, mfumo wa uzazi wa mwanamke, hedhi salama, mzunguko wa hedhi, pamoja na magonjwa ya zinaa na njia za kujikinga.
Ametaja manufaa ya mradi huo kuwa ni kuongeza uelewa sahihi, kujiamini kwa wasichana, kupunguza utoro shuleni na kuongeza ufaulu.
Awali, Mkurugenzi wa shirika hilo, Eliwilimina Buberwa, amesema lilianzishwa mwaka 2019 likiwa na lengo la kusaidia watoto wa kike waliopo pembezoni mwa miji kupata haki yao ya msingi ya elimu.
Amesema tangu kuanzishwa kwake, limefikia zaidi ya watoto 10,000 ndani na nje ya jiji la Arusha, na linaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuwafikia walioachwa nyuma.
