Kessy: Kukosekana Winifrida kumetuathiri JKT Queens

KOCHA wa JKT Queens, Kessy Abdallah amesema kukosekana kwa mshambuliaji wake tegemeo, Winifrida Gerald kumewaathiri kwa kiasi kikubwa kutokana na umuhimu wake katika safu ya ushambuliaji.

Winifrida anayeongoza kwa ufungaji wa mabao JKT Queens akiwa na manane, alifungiwa mechi tatu na faini ya Sh500,000 kwa kumshambulia beki wa Geita Queens.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kessy alisema Winifrida ni mchezaji anayebeba majukumu makubwa uwanjani na wachezaji wengine wamekuwa wakimtegemea kutafuta matokeo.

“Ni mchezaji muhimu tena sana, kimetuathiri kwa sababu hata wenzake wanamtegemea, kwa hiyo ilikuwa kazi kubwa sana kuwaelewesha kuwa tunaweza kufanya kitu bila yeye,” alisema Kessy.

Aliongeza changamoto kubwa haikuwa tu kiufundi bali pia kisaikolojia kwa wachezaji wengine, ambao walipaswa kujijenga upya kujiamini na kucheza kwa mshikamano zaidi.

Kocha huyo alisema baada ya kufanya kazi ya kuwajenga kifikra, wachezaji wake walielewa na kuanza kuonyesha mabadiliko chanya uwanjani.

“Baadae walinielewa na kweli tumeweza kufanya vizuri michezo miwili bila yeye na nashukuru Mungu na tunaamini tutafanya vizuri,” aliongeza.

Pamoja na mafanikio hayo, Kessy alikiri ushindani katika mechi zao umekuwa mkubwa, huku kila timu ikipambana kwa nguvu kutafuta ushindi.

“Vijana wana ari kubwa wanapambana, ila nikiri tu mechi zetu zimekuwa na upinzani mkubwa sana.”

JKT iko nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi na pointi 32 kwenye mechi 13 ilizocheza hadi sasa.