Yanga Princess waomba subira, waahidi kurudi kwenye ubora

MRATIBU wa Yanga Princess, Kibwana Matokeo amewataka mashabiki wa timu hiyo kuendelea kuwa na subira baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo, kwani bado wana nafasi kubwa ya kuwania ubingwa wa ligi.

Yanga Princess iliyopo nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi na pointi 33, imepoteza mechi mbili dhidi ya Simba Queens na Tausi FC.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kibwana alisema matokeo hayo hayakuwa ya kufurahisha, lakini ni sehemu ya mchezo na wanajipanga kurejea kwa nguvu katika mechi zijazo.

“Tulipoteza mechi mbili, haikuwa siku nzuri kwetu, lakini tunaomba mashabiki wavumilie. Tunafanya kazi kubwa kuhakikisha mechi zijazo tunafanya vizuri,” alisema Kibwana.

Aliongeza licha ya kupoteza michezo hiyo, bado ligi haijaisha na kuna michezo mingi iliyobaki ambayo inaweza kubadilisha mwelekeo wa mbio za ubingwa.

“Bado tuna mechi nyingi mbele yetu ambazo zitatupa taswira halisi ya kupambania ubingwa. Tunawaomba mashabiki waendelee kutusapoti na InshaAllah tutarudi kwenye ubora wetu,” aliongeza.

Matokeo hayo yanaifanya Yanga Princess kubaki katika nafasi ya pili na kupunguza gepu la ubingwa dhidi ya Simba Queens.