Athari za watoto kuingia kwenye ajira hatarishi

Simiyu. Licha ya juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali pamoja na wadau wa maendeleo kulinda haki za watoto, bado baadhi yao katika jamii wanaendelea kuingia kwenye ajira hatarishi.

Wakizungumza leo Aprili 12, 2026 na Mwananchi digital wadau wa masuala ya watoto mkoani Simiyu wamesema kuwa katika baadhi ya maeneo ya vijijini na miji midogo, watoto wamekuwa wakionekana kujihusisha na kazi nzito kama vile kubeba mizigo mizito sokoni, kufanya kazi mashambani kwa muda mrefu, kuuza bidhaa barabarani au kufanya kazi katika mazingira yasiyo salama.

Wanasema ajira za aina hiyo mara nyingi huwanyima watoto haki yao ya msingi ya kupata elimu, kupumzika na kukua katika mazingira salama.

Mkazi wa Lamadi katika Wilaya ya Busega, Jackson Bura amesema wakati mwingine hali ngumu ya maisha huwafanya baadhi ya wazazi kuruhusu watoto wao kufanya kazi ili kusaidia kipato cha familia.

Baadhi ya watoto wakifanya kazi hatarishi kwenye maeneo ya mgodini.Picha na mtandaoni

“Kuna familia ambazo zina kipato kidogo sana. Wazazi wengine huona ni bora mtoto akaenda kufanya kazi ili kusaidia mahitaji ya nyumbani,” amesema.

Ofisa Maendeleo ya Jamii wilayani Maswa anayeshughulika na watoto, Basila Bruno ameonya kuwa ajira hatarishi kwa watoto inaweza kuwa na athari kubwa kwa maendeleo yao ya kimwili, kiakili na kielimu.

Amesema kuwa watoto wanaojihusisha na kazi nzito au hatarishi mara nyingi hukosa muda wa kusoma au hata kuacha kabisa shule na wengine hukumbana na hatari za kiafya au ajali kutokana na mazingira wanayofanyia kazi.

Mwalimu wa Shule ya Msingi Mwandoya iliyopo  wilayani Meatu, Paulina Joseph amesema baadhi ya wanafunzi hushindwa kuhudhuria masomo kikamilifu kwa sababu ya majukumu ya kazi wanayofanya baada ya muda wa shule.

“Unakuta mtoto anakuja shule akiwa amechoka sana kwa sababu amefanya kazi nzito asubuhi au jioni. Hali hiyo inaathiri uwezo wake wa kujifunza,” amesema.

Naye Mwanasheria, Daud Masunga amesema kuwa kwa mujibu wa sheria za kazi na sheria za mtoto nchini Tanzania, watoto hawaruhusiwi kufanya kazi zinazoweza kuhatarisha afya, usalama au maendeleo yao.

Mmoja wa watoto akifanya kazi kazi katika mgodi wa dhahabu mkoani Simiyu. Picha na Maktaba

“Sheria hizo pia zinalenga kuhakikisha watoto wanapata haki yao ya msingi ya elimu na ulinzi, hata hivyo, changamoto kubwa imekuwa katika utekelezaji wa sheria hizo, hasa katika maeneo ya vijijini ambako uelewa wa haki za mtoto bado ni mdogo kwa baadhi ya wananchi,” amesema.

Maingu John, mtaalamu wa masuala ya maendeleo ya ukuaji wa watoto, amesema kuwa kupambana na tatizo la ajira hatarishi kunahitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali wakiwemo wazazi, viongozi wa jamii, walimu pamoja na vyombo vya Serikali vinavyosimamia ustawi wa jamii.

Anasema wazazi wanapaswa kutambua wajibu wao wa kulinda na kuendeleza ustawi wa watoto, huku viongozi wa jamii wakihimizwa kutoa elimu na kuchukua hatua pale wanapoona watoto wakifanyishwa kazi zisizofaa.

Mkuu wa divisheni ya Maendeleo ya Jamii katika halmashauri ya Mji wa Bariadi, Rogers Lyimo amesema kuwa Serikali kupitia idara za maendeleo ya jamii na kazi inatarajiwa kuendelea kusimamia utekelezaji wa sheria na kutoa elimu kwa jamii kuhusu madhara ya ajira hatarishi kwa watoto.