Tanga. Baadhi ya wanafunzi katika Shule ya Msingi Churwa iliyopo Kata ya Muhinduro, Tarafa ya Maramba wilayani Mkinga mkoani Tanga, wanalazimika kujifunzia chini ya miti kutokana na uhaba mkubwa wa madarasa hali inayowaathiri kitaaluma na kupunguza ufanisi wa ujifunzaji wao.
Shule hiyo ina vyumba vinne tu vya madarasa ya zamani visivyokidhi idadi ya wanafunzi zaidi ya 600 waliopo, huku ujenzi wa madarasa mapya manne ukiendelea kwa kusuasua kwa muda mrefu bila kukamilika jambo linalozidi kuongeza tatizo hilo kwa wanafunzi.
Wakazi wa kijiji cha Churwa wamelazimika kufikisha malalamiko yao Chama cha Mapinduzi, CCM Mkoa wa Tanga, wakiiomba iingilie kati baada ya jitihada zao za muda mrefu kushindikana.
Akizungumzia changamoto hiyo mkazi wa kijiji hicho Seif Killo amesema watoto wao wanateseka kwa kutegemea miti kama sehemu ya kujifunzia, hali inayowafanya washindwe kupata mazingira bora ya elimu wanayostahili.
“Watoto wetu wanategemea vivuli vya miti, jua likiwaka ni lao na mvua ikinyesha ni yao hali hii inawafanya washindwe kusoma kwa utulivu,” amesema Killo.
Ameongeza kuwa matarajio yao ni kuona madarasa yanakamilika kwa wakati ili kuboresha mazingira ya elimu kwa watoto wao, kwani mazingira mazuri huchochea ufaulu na ari ya kujifunza kwa wanafunzi.
Kwa upande wake Salimu Hassan amelalamikia kasi ndogo ya ujenzi licha ya wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo, hali inayowaumiza kuona juhudi zao hazizai matunda.
Ameongeza kuwa uwepo wa mafundi wachache unachangia kuchelewesha kukamilika kwa mradi huo, hali inayoashiria ukosefu wa umakini katika utekelezaji wa mradi huo muhimu kwa jamii.
Kamati ya siasa ya CCM Mkoa wa Tanga ikiongozwa na mwenyekiti wake Rajab Abdurahman Abdullah katika shule ya Msingi Churwa katika wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga inayolalamikiwa kuchelewa kukamilika na kusababisha adha kwa wanafunzi. Picha na Mbonea Herman
“Tunaona mafundi wawili tu kila siku jambo linaloonyesha wazi kuwa kazi hii haijapewa kipaumbele kinachostahili,” amelalama mwananchi huyo.
Naye mkazi mwingine Ramadhan Waziri, amesema hali hiyo imewafanya wanafunzi kukosa masomo hasa wakati wa mvua, kwani hakuna mahali salama pa kukaa wala kujifunzia ndani ya shule hiyo.
“Wakati wa mvua watoto wanaishia kwenda shambani badala ya darasani kwa sababu hakuna sehemu ya kukaa wala kujifunzia hali hii inaathiri elimu yao,” amesema Waziri.
Ameongeza kuwa kukosekana kwa mikutano ya hadhara kunachangia kushindwa kuwawajibisha wahusika, hali inayosababisha mradi huo kuendelea kuchelewa bila majibu ya kuridhisha kwa wananchi.
“Hata mikutano ya kijiji haifanyiki mara kwa mara ili kumhoji mzabuni na kupata majibu ya kuchelewa kwa mradi,” amesema waziri.
Ofisa Elimu Msingi wa Wilaya ya Mkinga, Omari Mashaka, amekiri kuwepo kwa changamoto ya ucheleweshaji wa mradi huo, akieleza kuwa tatizo kubwa ni mzabuni kushindwa kuleta vifaa kwa wakati.
“Fedha zipo lakini changamoto kubwa ni mzabuni kutokuleta vifaa kwa wakati hata mimi hali hii hainifurahishi na tunatazama namna ya kuchukua hatua ikiwemo kuvunja mkataba,” amesema Mashaka.
Afisa elimu Msingi Wilaya ya Mkinga, Omari Mashaka. Picha na Mbonea Herman
Kutokana na hali hiyo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Rajab Abdallah aliingilia kati na kuagiza usimamizi madhubuti wa mradi huo, ili kuhakikisha unakamilika kwa haraka na kuwanusuru wanafunzi na mateso wanayopitia.
“Hatutaki visingizio sio suala la mzabuni pekee hata usimamizi unaonekana kuwa na changamoto hakikisheni kila mmoja anatekeleza wajibu wake ili mradi ukamilike kwa wakati,” amesema Abdallah.
Amewataka pia watendaji wa halmashauri kuwajibika ipasavyo badala ya kulaumiana, akisema mazingira yanaonyesha wazi kuwa kuna mapungufu katika usimamizi wa mradi huo.