Arusha. Walinzi sita wa jadi, “Sungusungu”, waliokuwa wamehukumiwa adhabu ya kifo mwaka 2024, wameachiliwa huru na Mahakama ya Rufani kwa kuwa mashtaka dhidi yao hayakuwa yamethibitishwa kwa viwango vinavyokubalika kisheria.
Kesi hiyo inahusiana na tukio la kifo cha Njokuti Moringe, maarufu kama Mbaazi, ambaye mwili wake ulipatikana Septemba 19, 2020, katika eneo la Kazingumu, Kijiji cha Kiteto, Wilaya ya Kiteto, ukiwa umezikwa nusu kwenye mchanga katika eneo lenye vilima na miteremko.
Kwa mujibu wa ushahidi wa Jamhuri, uliotegemea mashahidi 11 na vielelezo kadhaa, yakiwamo maelezo ya onyo ya washtakiwa, mwenyekiti wa kijiji hicho, Halid Swaya, aliyekuwa shahidi wa nne, ndiye aliyetoa taarifa ya tukio hilo kwa polisi.
Yeye pia alishuhudia mwili wa marehemu ukifanyiwa uchunguzi na shahidi namba moja, Dk Hassan Mkwachu wa kituo cha afya Enguselo, na pia alishuhudia ramani ya eneo la tukio ikichorwa na polisi, pamoja na kushuhudia maziko ya marehemu.
Kulingana na ushahidi wa Dk Mkwachu, mikono, miguu na shingo ya marehemu ilikuwa imefungwa kwa kamba, na mwili ulikuwa na majeraha kichwani, usoni na mikononi, alishambuliwa na kitu chenye ncha kali na alikufa siku saba nyuma.
Shahidi wa pili, ambaye alikuwa mpelelezi wa kesi hiyo, G.5310 Koplo Mussa, alieleza katika upelelezi wake kuwa aligundua waliotekeleza mauaji hayo walikuwa wanachama wa kikundi cha Sungusungu wa Kijiji cha Laalaa.
Alidai kuwa taarifa hiyo ilimsaidia kumkamata mrufani wa nne, Amini Masilimu, aliyekamatwa Septemba 20, 2020, ambaye ilidaiwa kukiri kushiriki mauaji na kuwataja washirika wake, wakiwamo warufani namba 1, 2, 3, 5 na 6.
Kwa mujibu wa shahidi huyo, warufani hao walikamatwa, na alidai kuwa Septemba 26, 2020, mrufani huyo wa nne aliwapeleka yeye na mashahidi namba 3, 4 na 5 hadi nyumbani kwake, ambapo ilipatikana simu ya kiganjani iliyodaiwa kuwa ni ya marehemu.
Katika shauri hilo, upande wa Jamhuri ulitoa maelezo ya onyo ya warufani watano waliodaiwa kukiri kufanya mauaji hayo, na kwamba maelezo hayo yaliandikwa na mashahidi namba 7, 8, 11, 10 na 9, ambao ni askari polisi.
Ilidaiwa kuwa mrufani wa kwanza, Samwel Mgomelwa, ndiye aliyetoa amri ya kukamatwa kwa marehemu kwa tuhuma kuwa alikuwa akisababisha vurugu katika duka lake la kuuza pombe (pombe shop) au alikuwa mwizi wa ng’ombe.
Warufani wote walikanusha tuhuma dhidi yao, na kila mmoja alieleza namna alivyokamatwa na polisi, kutendewa mambo yasiyo ya haki, kupigwa na kulazimishwa kukiri kutenda kosa na kusaini maelezo hayo ya onyo.
Baada ya kusikiliza ushahidi wa pande mbili, Machi 5, 2024, Jaji Gladys Barthy wa Mahakama Kuu, Kanda ya Babati, aliwatia hatiani washtakiwa sita kwa kosa la kumuua Moringe kwa kukusudia, na kuwaachia huru washtakiwa watatu.
Waliohukumiwa kifo na ambao jopo la majaji watatu, Lugano Mwandambo, Abraham Mwampashi na Lameck Mlacha, limewaachia huru ni Samwel Mgomelwa, Ramadhan Idd, Manda Ulinje, Amini Masilimu, Elia Lendama na Adason Chuyo.
Hawakuridhishwa na hukumu hiyo, hivyo wakakata rufaa katika Mahakama ya Rufani Tanzania, na katika kikao chake kilichofanyika jijini Arusha, jopo la majaji hao lilikubaliana na sababu za rufaa zilizowasilishwa na warufani pamoja na upande wa Jamhuri.
Katika usikilizwaji wa rufaa hiyo, warufani waliwakilishwa na jopo la mawakili sita wa kujitegemea ambao ni Hamis Mkindi, Daniel Lyimo, Kapimpiti Mgalula, Nicodemus Mbuga, Mwamili Mahimbali na wakili Ombeni Kimaro.
Jamhuri iliwakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Mary Lucas, ambaye majaji walipomuuliza msimamo wake, aliunga mkono rufaa hiyo kwa sababu moja tu, kwamba mashtaka dhidi ya warufani hayakuthibitishwa na hivyo kuacha mashaka.
Akijenga hoja, mmoja wa mawakili wa warufani, Mkindi, alieleza kuwa taratibu zilizotumika kupokea vielelezo namba P4, P5, P6, P7 na P8, ambavyo ni maelezo ya washtakiwa na ambayo mahakama iliyazingatia kuwatia hatiani, zilikiukwa.
Wakili huyo alieleza kuwa maelezo hayo ya warufani yalipokelewa kama ushahidi wakati wa kesi ndani ya kesi (trial within trial) na si kwenye kesi ya msingi, na kwa kuwa hayakupokelewa katika kesi ya msingi, maana yake hayakuwa ushahidi.
Hivyo aliomba vielelezo hivyo viondolewe katika mwenendo wa shauri hilo, na vikishaondolewa, basi kunakuwa hakuna ushahidi wa kuwatia hatiani warufani.
Kwa upande wake, wakili Mgalula alieleza kuwa mashtaka dhidi ya warufani hayakuthibitishwa kwa vile kulikuwa na tofauti kati ya ushahidi na maelezo ya kosa, kwani kosa linadaiwa kutendeka Kazingumu Lualaa, lakini ramani ya eneo la tukio iliyochorwa na mmoja wa mashahidi inataja eneo ni Kazingumu Partimbo.
Kwa pamoja, mawakili Mkindi, Mgalula na Kimaro walieleza kuwa maelezo ya onyo yaliyotumika kuwatia hatiani yalikuwa yanajikanganya, na kutoa mfano wa maelezo ya mrufani namba moja na mbili juu ya sababu za kuuawa kwa marehemu.
Mathalani, walisema wakati mrufani wa kwanza akidaiwa kueleza kuwa marehemu aliuawa kwa sababu ya kuleta vurugu eneo la kuuza pombe, mrufani namba mbili yeye katika maelezo yake alidai aliuawa kwa kuwa alikuwa mwizi wa ng’ombe.
Jamhuri ilivyounga mkono rufaa
Jamhuri iliwakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Mary Lucas, ambaye majaji walipomuuliza msimamo wake, aliunga mkono rufaa hiyo kwa sababu moja tu, kwamba mashtaka dhidi ya warufani hayakuthibitishwa na hivyo kuacha mashaka.
Wakili huyo alieleza kuwa kutiwa hatiani kwa warufani kulifanyika kimakosa kwa kuegemea maelezo ya onyo ambayo si ya kweli na hayana uungwaji mkono.
Alieleza kuwa kile kilichoitwa kukiri kosa kilichomo katika maelezo hayo hakikushabihiana na ushahidi uliotolewa mahakamani uliopo katika rekodi.
Alitolea mfano kuwa, kulingana na shahidi namba moja na kielelezo P1, marehemu alikuwa na majeraha ya kukatwa na kitu chenye ncha kali, lakini maelezo ya onyo yanadai kuwa walitumia fimbo na nondo kumshambulia marehemu.
Kwa mujibu wa wakili huyo, maelezo ya onyo ambayo hayaungwi mkono yanaweza kutumiwa tu kama yana ukweli, lakini katika rufaa iliyopo mbele ya mahakama, maelezo hayo ya ungamo hayakuwa ya kweli.
Pia alieleza kuwa haiwezi kusemwa kuwa mrufani namba nne, aliyekuwa mikononi mwa polisi, alikuwa mtu huru wakati akidaiwa alikiri mbele ya mashahidi namba 2, 3, 4 na 5, na kwamba ungamo lake hakulitoa kwa hiari, hivyo hayakubaliki.
Katika hukumu yao waliyoitoa Aprili 10, 2026, na kuwekwa katika tovuti ya mahakama Aprili 11, 2026, walisema hoja ya msingi ya kuamuliwa na mahakama hiyo ni kama kesi dhidi ya warufani ilithibitishwa pasipo mashaka ama la.
Hata hivyo, majaji walisema zipo hoja nne ambazo ni kupokelewa kwa maelezo ya washtakiwa wakati wa kesi ndani ya kesi, kuwepo mkanganyiko wa eneo la tukio na maelezo ya mdomo ya kukiri kosa ya mrufani namba nne.
Hoja nyingine ni uhalali wa kupokelewa kwa maelezo ya onyo ya warufani namba 1, 2, 3, 5 na 6 katika kesi ndani ya kesi, na hapakuwa na dosari kisheria.
Kuhusiana na maelezo ya mdomo ya kukiri kosa ya mrufani namba nne, walieleza kuwa hakuwa huru wakati akitoa maelezo hayo, kwani alikuwa chini ya ulinzi wa polisi na akiwa amefungwa pingu, hivyo wanachukulia hakukiri kosa.
Kuhusu kupokelewa kwa maelezo ya onyo ya warufani namba 1, 2, 3, 5 na 6, majaji hao walisema ukweli wa maelezo hayo unatia mashaka, kwani baadhi ya warufani walidai marehemu alikamatwa kwa sababu ya wizi wa ng’ombe, wengine wakisema vurugu.
“Zaidi ni kwamba, kulingana na mashahidi wa Jamhuri, hasa shahidi namba moja, walisema marehemu alikuwa na majeraha mwilini yaliyosababishwa na kukatwa na kitu chenye ncha kali, lakini warufani katika hayo maelezo yao ya onyo walidaiwa kueleza walitumia fimbo na nondo kumshambulia marehemu.”
“Mbali na kwamba maelezo yalichukuliwa chini ya kifungu 58 cha CPA na kubadilishwa kama kifungu cha 59, na hayakuwa na ukweli, lakini mbaya zaidi hayakuchukuliwa kama sheria inavyotaka,” walieleza majaji hao.
Kwa mujibu wa majaji, endapo maelezo yanachukuliwa chini ya kifungu cha 59 cha CPA, mtuhumiwa anaandika mwenyewe maelezo yake, lakini katika maelezo yaliyopo mahakamani, yaliandikwa na polisi chini ya kifungu namba 59.
“Kwa kuwa maelezo ya warufani namba 1, 2, 3, 5 na 6 yalichukuliwa kinyume na kifungu hicho cha 59 cha CPA, hayakupaswa kupokelewa kama kielelezo. Ilikosewa kisheria kuyatumia kuwatia hatiani warufani, hivyo yanafutwa kwenye rekodi.”
Majaji hao walisema, baada ya maungamo ya mdomo ya mrufani wa nne kuondolewa, sambamba na kufutwa kwa maelezo ya warufani namba 1, 2, 3, 5 na 6, ushahidi unaobakia hautoshi kuwatia hatiani warufani, hivyo wanaachiwa huru.
