Sichone afurahia maisha Uarabuni | Mwanaspoti

MSHAMBULIAJI wa Kitanzania, Morice Sichone anayekipiga Gulf United inayoshiriki Ligi Daraja la Pili Falme za Kiarabu amesema amekuwa na wakati mzuri tangu ajiunge na timu hiyo.

Nyota huyo alijiunga na Gulf akitokea Trident FC ya Zambia alikocheza mechi 18 akifunga mabao sita na kutoa asisti nane.

Akizungumza na Mwanaspoti Sichone alisema tayari amefunga mabao matano na asisti mbili kwenye mechi nane.

“Tayari nimefunga mabao matano na kutoa asisti mbili katika mechi nane nilizocheza, hali ambayo inanipa motisha zaidi ya kuendelea kufanya vizuri,” alisema Sichone na kuongeza, mazingira ya timu hiyo ni mazuri na yanampa nafasi ya kuonyesha uwezo wake, huku akisisitiza ushindani uliopo katika kikosi hicho unamsaidia kupambana kila siku.

“Ushindani ni mkubwa lakini wachezaji wenzangu wananipa ushirikiano mkubwa na benchi la ufundi lina imani na mimi, jambo linalonifanya nijitume zaidi kila ninapopata nafasi.”