Arusha. Tanzania imetajwa kuwa na mafanikio makubwa katika kuboresha maisha ya wakulima wadogo wa kahawa.
Hilo limebainishwa na Umoja wa Wadau wa zao la Kahawa Duniani (ICP) wakati ukitimiza miaka 25 tangu kuanzishwa kwake, ambapo umeangazia mafanikio katika kuboresha maisha ya wakulima hao wadogo wa kahawa duniani.
Kwa mujibu wa Morgan Mkonyi, Meneja Mwenza wa Shirika la Hanns R. Neumann Stiftung (HRNS) Tanzania, mafanikio ya ICP yanaonekana moja kwa moja katika maisha ya wakulima wa kahawa nchini.
“Kwa Tanzania, miaka 25 ya ICP si tu kumbukumbu ya mafanikio, bali ni ushahidi wa mabadiliko halisi katika maisha ya wakulima wadogo. Kupitia mafunzo, ushirikiano na uwekezaji wa muda mrefu, wakulima wameongeza uzalishaji, wameimarisha ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, na wameboresha maisha yao kwa ujumla,” amesema Mkonyi.
Ameongeza maadhimisho hayo pia ni fursa ya kuendeleza dhamira ya kuwawezesha vijana kuingia na kunufaika na sekta ya mnyororo wa kahawa.
Tofauti na miradi mingi ya kilimo inayolenga uzalishaji pekee, ICP imekuwa ikitekeleza mkakati wa jumla unaojumuisha nyanja mbalimbali za maisha ya mkulima.
Mbinu hiyo inahusisha maendeleo ya biashara za familia, uimarishaji wa vikundi vya wakulima, usawa wa kijinsia, ushiriki wa vijana, pamoja na mbinu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Tangu kuanzishwa kwake, zaidi ya familia 125,700 za wakulima katika nchi 13 zinazozalisha kahawa zimefikiwa na miradi ya ICP.
Wakulima wamewezeshwa kutumia mbinu bora za kilimo, pamoja na kupanua shughuli zao kwa kulima mazao mengine ili kuongeza usalama wa chakula na kipato cha ziada.
Aidha, ICP imechangia kuanzishwa na kuimarishwa kwa zaidi ya vyama na ushirika wa wakulima 2,700, hatua iliyowawezesha kupata huduma muhimu na soko lenye ushindani.
Aidha, katika juhudi za kuhakikisha ushirikishwaji, ICP imeweka mkazo katika kuwawezesha wanawake na vijana kushiriki kikamilifu katika uamuzi.
Takwimu za mwaka 2025 zinaonesha asilimia 45 ya washiriki wa mafunzo walikuwa wanawake, huku asilimia 22 wakiwa vijana wenye umri wa kati ya miaka 18 hadi 35.
Kwa mujibu wa Rui Miguel Nabeiro, Mwenyekiti wa kamati ya uongozi ya ICP, ushirikiano huo umefanikiwa kwa sababu ya kuunganisha maarifa, rasilimali na uzoefu kwa lengo la pamoja la kuboresha maisha ya wakulima.
Katika kipindi cha miaka 25, wanahisa sita wa ICP wamewekeza Euro milioni 25 katika shughuli za ICP, na kuvutia rasilimali za ziada kutoka mashirika ya wafadhili na washirika wengine ili kuendeleza suluhisho zenye ufanisi zinazoleta mabadiliko ya kweli na yenye tija katika sekta ya kahawa.
Hata hivyo, licha ya mafanikio hayo, sekta ya kahawa bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali, zikiwemo mabadiliko ya tabianchi, kupanda kwa gharama za uzalishaji, pamoja na kupungua kwa misaada ya kimataifa katika baadhi ya nchi.
Kutokana na hali hiyo, ICP imeeleza itaendelea kushikilia mkakati wake wa muda mrefu wa uwekezaji na ushirikiano, ili kuhakikisha mabadiliko endelevu katika sekta ya kahawa yanaendelea kupatikana.
Kwa ujumla, mafanikio ya ICP ndani ya miaka 25 yanaifanya Tanzania kuwa mfano hai wa namna ushirikiano wa kimataifa unavyoweza kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya kilimo na maisha ya jamii za wakulima.
