Babati. Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Regina Ndege, amewataka askari wanawake wa vyombo vya ulinzi na usalama wa Mkoa wa Manyara kuchangamkia fursa za kiuchumi ili wajiongezee kipato badala ya kutegemea mishahara pekee.
Hata hivyo, amewaonya askari hao kujiepusha na mikopo umiza yenye riba kandamizi inayohusisha kuacha kadi za kielektroniki za benki, na badala yake kugeukia mikopo ya riba nafuu inayopatikana katika taasisi za fedha za Serikali na binafsi zinazotambulika kihalali.
Naibu Waziri Ndege ameeleza hayo mjini Babati leo, Aprili 12, 2026, kwenye siku ya askari wanawake wa vyombo vya ulinzi na usalama Mkoa wa Manyara, yenye kauli mbiu isemayo: “Nidhamu, haki, weledi na uadilifu, msingi wa mafanikio yao.”
Akizungumza wakati akifungua mafunzo ya uwezeshaji, kuongeza ufanisi, kuimarisha uongozi na kujenga uchumi kwa wanawake wa vyombo vya ulinzi na usalama Mkoa wa Manyara, amewaasa wajinyanyue kiuchumi.
“Ninawahimiza askari wanawake wa vyombo vya ulinzi na usalama Mkoa wa Manyara kuchangamkia fursa mbalimbali za kiuchumi kama wanawake wengine ili kuongeza kipato badala ya kutegemea mishahara pekee,” amesema Naibu Waziri Ndege.
Ameeleza kwamba ni muhimu askari hao wanawake kufahamu mipango na mikakati ya kujiinua kiuchumi kihalali, kwa sababu kutegemea mishahara pekee si vyema kwani haitoshelezi mahitaji ya kila siku.
“Nawashauri muache kuingia kwenye mikopo umiza na kandamizi ambayo inalazimisha kuacha kadi za benki, badala yake muwe wabunifu wa kuchangamkia fursa mbalimbali za kiuchumi zilizoidhinishwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan,” amesema Naibu Waziri Ndege.
Pia, amewahimiza kuendelea kushirikiana na jamii katika kujenga ulinzi na usalama, mtandao imara, na kupambana na ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto.
Mwenyekiti wa mtandao wa polisi wanawake Mkoa wa Manyara, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Christina Mkonongo, amesema umoja wa askari wanawake wa vyombo vya ulinzi na usalama Mkoa wa Manyara umekuwa chachu ya ushirikiano wa kiutendaji wa kila siku katika matendo ya huruma kwa jamii.
“Mheshimiwa Naibu Waziri, tunashukuru kwa kuja kwako kwani umetujengea uwezo zaidi kupitia nasaha zako, na sisi askari wanawake wa vyombo vya ulinzi na usalama Mkoa wa Manyara tunaahidi kutekeleza hayo,” amesema SSP Mkonongo.
Mkuu wa Polisi Wilaya ya Babati, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Ernesta Mwambinga, amesema lengo lao kuu ni kujengea uwezo askari wa kike mkoani humo katika nyanja za kiuchumi, kiafya na kuelewa masuala mbalimbali ya mahusiano.
“Akiangalia dunia ilivyo sasa, sera ya nchi inatutaka kujenga uchumi kuanzia mtu mmoja mmoja, na askari kama wanawake wengine wanahitaji kuimarisha uchumi na kujua mipango ya utunzaji wa fedha,” amesema SSP Mwambinga.
Ameeleza kwamba wanawake wanapokuwa katika hali nzuri ya kiuchumi na kifedha wataweza pia kuihudumia jamii kwa weledi na usafi.
Mwenyekiti wa mtandao wa askari wanawake wa Magereza Mkoa wa Manyara, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza (SSP) Elizabeth Morembwa, amesema mafunzo hayo yatasaidia kuimarisha utoaji wa huduma za kurekebisha tabia za wafungwa.
SSP Morembwa amesema kiutendaji itasaidia kujenga uwezo wa kujiamini kwa watumishi na kutekeleza majukumu yao katika kazi ya kuwarekebisha wafungwa ili wanapotoka wawe raia wema.