HATIMAYE mzunguko wa 22 wa Ligi Kuu Zanzibar umemalizika kwa timu ya KVZ kurejea kileleni mwa msimamo ikiiondoa Fufuni iliyodumu kwa wiki moja katika nafasi hiyo.
KVZ imeweka utawala wake baada ya kuitandika Malindi mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Mao A kisiwani Unguja katika mechi iliyochezwa April 11, 2026, saa 10:15 jioni, sasa ipo kileleni na pointi 43, ikifuatiwa na Fufuni yenye 41 kabla ya JKU haijacheza na Zimamoto zote zikiwa na pointi 39.
Mzunguko huo umehitimishwa Jumapili kwa mechi moja kati ya Zimamoto na JKU, huku kukiwa na presha kwa timu zote 16 zinazoshiriki Ligi Kuu Zanzibar zilizopo kwenye hekaheka za kuwania ubingwa, nyingine zikijinusuru kushuka daraja.
Katika mzunguko wa 23 unaotarajiwa kuanza Jumamosi April 18, 2026, utakuwa ni miongoni mwa mechi nne zitakazotoa uamuzi kwa nne bora na zitakazoshuka daraja.
Mzunguko huo wa 23 utaanza kwa michezo miwili ambapo, bingwa mtetezi wa ligi hiyo, Mlandege atafungua pazia akiikaribisha Muembe Makumbi kwenye Uwanja wa Mao A.
Hesabu zilivyo, Mlandege ina wakati mgumu wa kutetea ubingwa ikiwa nafasi ya saba ikikusanya pointi 34 na Muembe Makumbi inashika nafasi ya nane. Zilipokutana duru la kwanza, timu hizo zilitoa suluhu ya 0-0.
Katika mchezo mwingine, Fufuni itakuwa mwenyeji wa Junguni United kwenye Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba, awali timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.
Aprili 19, kutakuwa na michezo mitatu, New Stone Town vs Chipukizi ambazo duru la kwanza Chipukizi iliibuka na ushindi wa bao 1-0, Polisi itapambana na KVZ, wenyeji wakiwa na kumbukumbu ya kuchapwa mabao 2-1 na KVZ duru la kwanza, kisha Mafunzo dhidi ya New King ambazo duru la kwanza zilitoka sare ya mabao 2-2.
April 20, JKU itavaana na Kipanga (Kipanga iliitandika JKU bao 1-0 katika duru la kwanza), huku Zimamoto ikitoana jasho na Uhamiaji, wakati KMKM dhidi ya Malindi zitahitimisha mzunguko huo Mei Mosi.