Watatu wadaiwa kulawitiwa Igunga Tabora | Mwananchi

Tabora. Watu Watatu wakazi wa Wilaya ya Igunga, mkoani Tabora wanadaiwa kulawitiwa na mtumishi wa halmashauri ya wilayani humo kwa nyakati tofauti.

Akizungumza na Mwananchi leo Aprili 12, 2026 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao amesema wanaodaiwa kulawitiwa, wawili ni wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya kutwa ya Igunga (17) na (18) na mmoja ni fundi pikipiki wilayani humo.

“Inadaiwa mtumishi huyu amekua akiwafanyia vitendo hivyo mara kadhaa hao wanafunzi pamoja na huyu fundi pikipiki ambaye ni mkazi pia wa hapo hapo Igunga,” amesema Kamanda Abwao.

Amesema mtumishi huyo ambaye anafanya kazi halmashauri ya Igunga upande wa utawala na mkazi wa mtaa wa Stoo Igunga mjini, anashikiliwa na Jeshi la Polisi Tabora kwa ajili ya mahojiano zaidi ikiwa ni pamoja na uchukuaji wa sampuli kwa ajili ya uchunguzi wa kisayansi kwa pande zote mbili.

Amebainisha kuwa mbinu aliyokua akiitumia mtuhumiwa ni kuwarubuni na vitu tofauti na kuwapa fedha anapowahitaji.

“Tumefanya mahojiano ya awali na uchunguzi wa awali pia umefanyika, kuna baadhi ya vitu tumebaini lakini tunaendelea na uchunguzi kubaini tatizo zaidi ili tuweze kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria,” amesema.

Amesema matukio hayo yanadaiwa kutekelezwa katika kipindi cha Desemba 2025 hadi Aprili 6 2026, katika nyakati tofauti na maeneo tofauti wilayani humo.

Kamanda huyo ametoa wito kwa wananchi wa Tabora kuchukua tahadhari na kuacha kurubuniwa na vitu ambapo inapelekea kuharibu utu na heshima yao.

“Haiwezekani unakubali kirahisi kufanyiwa vitu vya ajabu na hutoi taarifa, unakuwa umeridhika tu na hela ndogo ambazo pia hazileti matokeo yoyote kwenye maisha yenu.”

Amewahimiza wazazi na walezi kuhakikisha wanafanya ufuatiliaji wa karibu kwa watoto wao ili kubaini vitendo hivi kwa haraka vinapojitokeza, hasa ikizingatiwa vijana hao wawili ni wanafunzi wa kidato cha nne ni nguvu kazi ambayo inapaswa kurudi kuleta matokeo kwenye jamii.

“Lindeni watoto na wafuatilieni na mkiona mambo ambayo hamuyaelewi tupeni taarifa mapema tuchukue hatua, msisubiri mpaka tatizo liwe kubwa lakini pia msipende kumaliza kesi nyumbani kwa matukio kama haya,” amesema Kamanda Abwao.