Kundemba, Black Sailors vita ya FA Cup Unguja

ILE vita ya Ligi Daraja la Kwanza Kanda ya Unguja, sasa inahamia kwenye Kombe la Shirikisho (FA Cup) kwa Black Sailors kupambana na Kundemba.

Kwa kawaida timu hizi zinapokutana zimekuwa na ushindani wa aina yake na mara mwisho zilitoana jasho kwenye ligi kwa sare mabao 2-2.

Mechi hiyo ya hatua ya 16 bora, imepangwa kuchezwa Jumatatu hii Aprili 13, 2026 kwenye Uwanja wa Mao A kisiwani Unguja kuanzia saa 10:00 jioni.

Nahodha wa Black Sailors, Iddi Idrissa Iddi, alisema kikosi chao kimejipanga kuhakikisha kinapata ushindi katika mchezo wa Kombe la FA dhidi ya Kundemba ili kusonga mbele.

Akizungumza baada ya mazoezi ya kujiandaa na mchezo huo, pamoja na mechi za ligi, Iddi alisema lengo lao ni kushinda michezo yote iliyopo mbele yao ili kufikia malengo ya kutwaa ubingwa msimu huu.

Alisema, maandalizi yao yanaendelea vizuri na wachezaji wako katika hali nzuri ya ushindani, jambo linalowapa matumaini ya kufanya vizuri katika mchezo huo muhimu.

“Tupo katika maandalizi makini kwa ajili ya mchezo wa Kombe la FA pamoja na ligi, ili kujiweka sawa na kutimiza malengo yetu ya kutwaa ubingwa wa mashindano haya pamoja na Ligi Daraja la Kwanza Kanda ya Unguja,” alisema Iddi.

Aliongezea kuwa, ushindani katika mashindano hayo ni mkubwa, lakini wana imani na uwezo wa kikosi chao katika kuhakikisha wanapata matokeo chanya.