Dar es Salaam. Katika kukabiliana na mabadiliko mapya ya kiuchumi duniani, Wizara ya Vijana yaja na shindano la ‘Uchumi Challenge’, lengo likiwa kupata mawazo mbadala kutoka kwa vijana ya njia gani za kukabiliana na changamoto hizo.
Shindano hilo limetangazwa jana Aprili 11, 2026 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, katika mkutano wake na waandishi wa habari.
Nanauka alisema wamekuja na shindano hilo kutokana na kuwepo na mabadiliko mapya ya kiuchumi duniani ambayo kwa namna nyingine pia yameathiri uchumi wa mataifa mengine, hususani nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania katika sekta mbalimbali.
“Hata hivyo katika mabadiliko hayo mataifa mengi yamechukua hatua ya kuanza kujenga uchumi wao ambao unaweza kuzuia na kuikabili misukosuko ya kimataifa.
“Katika uchukuaji hatua hizo wamejikita katika kuimarisha maeneo kama uzalishaji wa ndani, kuwekeza katika ubunifu na teknolojia na kushirikisha wananchi wake kikamilifu katika kukabiliana na changamoto hizo.
“Kwa Tanzania hali hii inaleta umuhimu mkubwa wa kutumia rasilimali ya vijana ambayo ni nguvu kazi kubwa katika Taifa ambao ni asilimia 55.6. Kati yao wakiwa na miaka 15 mpaka 35 ambapo tuna tambua wana ubunifu, wanaweza kuleta fikra mpya na kuleta mtazamo mpana hasa kwenye mabadiliko yanayoendelea ndani na nje ya nchi,” alisema Waziri Nanauka.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, akiitambulisha kamati ya mashindano ya ‘Vijana Uchumi’ katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika, jijini Dar es Salaam
Amesema shindano hilo litatoa jukwaa la Kitaifa kwa vijana wa Kitanzania kutoka pande zote za nchi kwa kutoa mawazo ya ubunifu yanayotekelezeka lakini pia yanayohusu dira ya maendeleo 2050 na kuleta mawazo endelevu katika kulinda na kukuza uchumi wa Taifa, dhidi ya athari ya misukosuko ya dunia.
Alifafanua kuwa swali muhimu katika shindano hilo ni ‘Linapotokea tishio la uchumi wa dunia kushuka kutokana na misukosuko ya kimataifa ikiwemo vita, ushindani wa kiuchumi na teknolojia ni changamoto zipi zinazoweza kuikumba Tanzania na nini kifanyike ili uchumi wa Tanzania uendelee kuimarika?’
Kwa kutambua umuhimu wa shindano hili, Waziri Nanauka amesema Wizara imetenga takribani Sh50 milioni zitakazotolewa kwa washindi.
Pia ili kuhakikisha shindano linakuwa la vijana wenyewe ameunda kamati ya vijana ya kitaifa ili kulisimamia hatua ya mwanzo mpaka mwisho.
Mambo itakayoyafanya kamati hiyo amesema ni pamoja na kuweka utaratibu wa namna ya kushiriki shindano hilo kwa mujibu wa mwongozo wa wizara, kuratibu mchakato mzima wa upokeaji wa mawazo, kutoa hamasa kwa vijana kushiriki na kuchagua majaji wa shindano.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu shindano la ‘Vijana Uchumi’
“Ni matumaini yangu vijana walioteuliwa katika kamati hiyo watahakikisha shindano hilo linakuwa wazi, jumuishi na halina upendeleo wowote.
“Hii itatusaidia kupata mawazo ya kukuza uchumi hasa katika kipindi hiki ambacho Taifa letu na mataifa mengine yanapitia nyakati ambazo haziwezi kukabilika,” alisema Nanauka.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya vijana iliyoteuliwa, Joseph Malekela, ameahidi kufanya kazi kwa uwazi na uaminifu mkubwa kama alivyowataka waziri huyo, huku akiwataka vijana kuchangamkia fursa hiyo.
Wakati mmoja wa wajumbe, Chrispina Kabale, amesema wanashukuru wizara kuwaamini na kuwateua.
