Arusha. Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Fransisko, Padri Arnold Baijukua, amewataka Watanzania kumuenzi aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Sokoine, kwa kusimamia na kutekeleza usawa wa kiuchumi na kuhakikisha rasilimali za Taifa zinawanufaisha wananchi wote badala ya wachache.
Akizungumza leo Aprili 12, 2026 katika misa takatifu ya kumbukumbu ya miaka 42 tangu kifo cha Sokoine, iliyofanyika nyumbani kwake Monduli Juu mkoani Arusha, Paroko Baijukua, amesema njia sahihi ya kumuenzi kiongozi huyo ni kuendeleza misingi ya haki, uadilifu na kujali wanyonge.
Amesema Sokoine anakumbukwa kama mtetezi wa wanyonge aliyepinga vikali ulimbikizaji wa mali kwa wachache huku wengine wakikosa mahitaji ya msingi.
“Sokoine alisisitiza rasilimali za nchi ziwanufaishe wote, siyo wachache, hii ina maana hakuwa tayari kuona baadhi ya watu wanashiba huku wengine wakifa njaa,” amesema.
Baijukua ameongeza kuwa Sokoine alipambana dhidi ya rushwa, ulafi na maovu ya kijamii, akiamini kuwa haki ndiyo msingi wa amani ya kweli.
“Tunapomkumbuka leo, tuige mfano wake kwa vitendo. Tuwaelimishe watoto wetu maadili mema na kuwalea katika misingi ya uadilifu na huruma,” amesema.
Familia ya marehemu Edward Sokoine katika Misa takatifu ya kumbukumbu ya miaka 42 tangu kifo cha Sokoine, iliyofanyika nyumbani kwake Monduli Juu mkoani Arusha.
Amewataka viongozi wa sasa kuacha alama njema katika uongozi wao kwa kuendeleza misingi ya haki na uwajibikaji kama alivyoifanya Sokoine.
Katika hatua nyingine, Paroko Baijukua ameitaka Serikali kukamilisha ujenzi wa bwawa la Edward Sokoine alilolianzisha enzi za uhai wake, kwa lengo la kuvuna maji na kukabiliana na ukame katika eneo la Monduli Juu.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini, Steven Kiruswa, amesema Sokoine ataendelea kukumbukwa si tu na familia yake bali Taifa zima kutokana na mchango wake mkubwa.
“Kama si yeye nadhani hata mimi nisingekuwa hapa maana katika msako wake wa watoto wa Kimasai wapelekwe shule ndio na mimi nikachukuliwa na kusomeshwa, hatimaye leo nimekuwa Naibu Waziri,” amesema.
Naye Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, James Ole Milla, amesema Serikali inaendelea kutekeleza maono ya Sokoine kwa kuhakikisha kunakuwepo na usawa katika jamii na kuimarisha ustawi wa wafugaji.
Mbunge wa Monduli, Isaac Kapriano (Kadogoo), ameahidi kushughulikia maendeleo ya miundombinu ikiwemo bwawa na shule, pamoja na barabara katika kuenzi uadilifu wa kutatua changamoto za wananchi aliokuwa akiufanya kiongozi huyo, enzi ya uhai wake.
Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Gloria Kimath, amesema kuwa Serikali itaendeleza miradi yote yenye lengo la kuboresha maisha ya wananchi pamoja na kutatua migogoro ya ardhi.
Edward Moringe Sokoine alizaliwa Agosti 1, 1938 mkoani Arusha na kuwa Waziri Mkuu wa tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alitumikia nafasi hiyo kwa awamu mbili kuanzia Februari 13, 1977 hadi Novemba 7, 1980, na awamu nyingine kuanzia Februari 24, 1983 hadi Aprili 12, 1984 mauti yalipomkuta katika ajali ya gari eneo la Wami Dakawa (Dumila), mkoani Morogoro, akiwa na umri wa miaka 46.
