Mazungumzo ya Marekani, Iran yakikwama sintofahamu yatanda

Dar es Salaam. Hali ya usalama katika Mashariki ya Kati huenda ikaingia tena kwenye sintofahamu kufuatia kushindikana kwa mazungumzo yaliyolenga kupata suluhu ya mzozo unaoendelea katika ukanda huo.

Mazungumzo kati ya Marekani na Iran yaliyofanyika katika mji mkuu wa Pakistan, Islamabad, yameshindwa kufikia mwafaka baada ya majadiliano ya saa 21 mfululizo.

Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, amesema Iran imekataa masharti yaliyowekwa na upande wao.

Kushindikana kwa juhudi hizo za kidiplomasia kunazidisha hofu ya kurejea kwa mapigano, ambayo tayari yamekuwa na athari kubwa kiuchumi na kibinadamu katika eneo hilo.

Mzozo huo unahusisha mashambulizi yaliyoanzishwa na Marekani kwa kushirikiana na Israel dhidi ya Iran na kundi la Hezbollah lililopo nchini Lebanon, hali inayozidi kuongeza taharuki kuhusu mustakabali wa usalama wa kikanda na uchumi wa dunia.

Katika juhudi za kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano, Iran ambayo ndio inadhibiti Mlango Bahari wa Hormuz iliwasilisha masharti kadhaa, likiwemo la kukomesha vita katika nchi za Iraq, Lebanon na Yemen.

Aidha, ilitaka kusitishwa kabisa kwa uhasama dhidi yake bila kuwepo kwa ukomo wa muda, pamoja na kumalizwa kwa migogoro yote katika ukanda huo.

Masharti mengine yalihusu kufunguliwa upya kwa Mlango wa Bahari wa Hormuz kwa utaratibu maalumu utakaohakikisha uhuru na usalama wa usafirishaji wa nishati, kulipwa kwa fidia kamili kwa ajili ya ujenzi upya wa Iran, pamoja na kuondolewa kwa vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa dhidi yake.

Pia, Iran ilisisitiza kutolewa kwa fedha na mali zake zinazodaiwa kuzuiliwa nchini Marekani, ikiwa ni sehemu ya masharti ya kurejesha uhusiano wa kawaida wa kiuchumi.

Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kuondoka Islamabad, Vance aliyekuwa akiongoza ujumbe wa Marekani, alisema kushindikana kwa mazungumzo hayo ni pigo kubwa zaidi kwa Iran kuliko Marekani, akisisitiza kuwa mlango wa majadiliano bado upo wazi endapo masharti yatakayokubalika yatawasilishwa.

Alibainisha kuwa Iran imechagua kutokubali masharti yetu,” akisisitiza kuwa Marekani inahitaji kuona dhamira ya wazi kutoka Iran ya kutotengeneza silaha za nyuklia.

“Tunataka uthibitisho wa wazi kwamba hawatajaribu kumiliki silaha za nyuklia, wala zana zitakazowawezesha kufikia silaha hizo kwa haraka,” alisema Vance.

Mchambuzi wa siasa za kimataifa, Innocent Shoo amesema kushindwa kufikiwa kwa makubaliano ya kidiplomasia katika eneo la Mashariki ya Kati kunatoa taswira ya hali ya sintofahamu na mvutano unaoendelea kuongezeka.

Badala ya kujenga matumaini ya utulivu wa kudumu, amesema hali hii inaashiria uwezekano wa kurejea kwa mivutano ya kijeshi, siasa za nguvu, na ukosefu wa imani kati ya wahusika wakuu wa eneo hilo.

“Katika muktadha huu, swali muhimu linalojitokeza ni juu ya hatima ya kipindi cha wiki mbili cha usitishwaji wa mapigano kilichokuwa kimepangwa.

“Kukwama kwa mazungumzo kunaweka makubaliano hayo katika hatari kubwa ya kuvunjika, kwani usitishaji mapigano mara nyingi hutegemea mwendelezo wa mazungumzo na nia njema ya pande husika.”

“Bila msingi imara wa kisiasa, uwezekano wa kurejea kwa mapigano unabaki kuwa mkubwa, jambo ambalo linaweza kuathiri vibaya raia na miundombinu ya eneo hilo,” amesema.

Aidha, amesema Mlango Bahari wa Hormuz unaendelea kuwa kitovu cha taharuki ya kimkakati na sasa umejidhihirisha wazi kama kikwazo katika usafirishaji wa mafuta duniani.

Shoo amesema njia hii muhimu ya nishati imeendelea kuwa katika hali ya sintofahamu, jambo linalochangia kuvurugika kwa minyororo ya usambazaji wa mafuta.

Amesisitiza kuwa matokeo yake ni kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia, jambo ambalo linaambatana na ongezeko la bei za bidhaa na huduma kwa ujumla.

Kwa mujibu wa Shoo mnyororo huu wa athari unaanza kuonyesha dalili za kudorora kwa uchumi wa dunia, huku mataifa mengi yakikabiliwa na shinikizo la gharama za maisha na kupungua kwa kasi ya ukuaji wa kiuchumi.

“Kwa ujumla, kushindwa kwa makubaliano kunadhoofisha jitihada za amani na kuimarisha mazingira ya kutoaminiana.

“Mustakabali wa Mashariki ya Kati, katika hali hii, unaonekana kubaki katika mizani isiyotabirika, ukiwa umefungamanishwa na siasa za kimataifa, maslahi ya kiuchumi, na ushindani wa kijeshi unaoendelea kuunda sura ya eneo hilo,” amesema Shoo.