Mwanza. Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza limetao taarifa ya ajali ya gari iliyoua watu wawili ambao ni dereva na abiria iliyotokea katika Kijiji cha Igaka, barabara ya Sengerema–Geita.
Kamanda wa Jeshi la polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa amesema ajali hiyo ilihusisha gari aina ya Toyota Kluger na basi aina ya Tata na uchunguzi wa awali umebaini chanzo ni mwendo kasi wa dereva wa gari ndogo.
“Mwendo kasi wa gari ndogo Toyota Kluger uliosababisha dereva kushindwa kulimudu gari lake na kuhama njia,” amesema.
Aidha, amesisitiza kwa madereva na watumiaji wa barabara kuzingatia sheria za barabarani ili kuepuka ajali zinazoweza kuzuilika.
Kwa upande mwingine, Jeshi la Polisi limewakamata watu wawili kwa kosa la kujifanya maofisa wa Serikali na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Watuhumiwa hao ni Azizi Makongoro (45), mfanyabiashara na mkazi wa Kisesa, Wilaya ya Magu na Venance Mininga (42), mfanyabiashara na mkazi wa CapriPont, Wilaya ya Nyamagana.
Kamanda Mutafungwa amesema waliwakamata Aprili 09, 2026 saa 02:00 usiku eneo la Trapia Hotel, Wilaya ya Nyamagana na uchunguzi kuhusu tukio hili bado unaendelea.
“Watuhumiwa wamekuwa wakitenda makosa hayo kwa kuwalaghai wananchi wenye shida mbalimbali zinazohusisha taasisi za Serikali na kuwa wanaweza kuwasaidia huku wakidai wapatiwe fedha ili watoe msaada,” amesema.
Pia Mutafungwa amewaasa wananchi kufuata taratibu rasmi wanapohitaji huduma katika taasisi za umma na kuepuka kufanya miamala na watu wasio rasmi.