Dodoma. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amewataka Watanzania kutokuwa na hofu kuhusu suala la mafuta akisema Tanzania ipo macho na itahakikisha hakutokei madhara ya kukosekana kwa mafuta.
Amesema kuwa Serikali imekuwa na mikakati na mipango ya mara kwa mara ikiwamo kufanya vikao na sekta husika ili kuona namna Bora ya kuhakikisha mafuta hayaadimiki na wala bei hazipandi zaidi.
Ametoa kauli hiyo leo Jumapili Aprili 12,2026 wakati akizungumza na wananchi wa Vijiji vya Mvumi, Wilaya ya Chamwino na Kikombo katika Jiji la Dodoma kwenye ziara ya ukaguzi wa ujenzi wa Barabara ya Ntyuka – Mvumi – Kikombo.
Dk Mwigulu amekiri kuwa kutakuwepo na madhara siyo kwa Tanzania pekee bali yataikumba dunia yote kutokana na hali ilivyo hivyo akaomba Watanzania wasigombane wao kwa wao.
“Tunafanya vikao vya mara kwa mara kati ya wadau na Serikali ili kuwa na tathimini ya pamoja na kila hatua tutaendelea kutoa taarifa ya nini kinaendelea,” amesema Dk Mwigulu.
Mwishoni mwa wiki katika mkutano unaoendelea ndani ya ukumbi wa Bunge, Spika aliitisha vikao kwa ajili ya kujadili mambo ya mafuta.
Kikao hicho kiliwahusisha Waziri Mkuu, Waziri wa Nishati, Spika wa Bunge, Kamati ya Nishati na wataalam na kilifanyika Ofisi ya Spika iliyopo ndani ya jengo la Bunge.
Amewataka Watanzania kuwapuuza aliowaita wanajitokeza mara kwa mara kuwafanya wananchi waingie kwenye taharuki kitu ambacho hakikupaswa kufikia hapo badala yake wanajinufaisha wenyewe kwa masilahi yao.
Amesema Watanzania wanapaswa kuwa watulivu hasa zinapotokea siasa za kimataifa na kutaka kila Mtanzania kuwa mlinzi wa rasilimali za nchi na kukumbusha kauli yake alipoteuliwa kwa mara ya kwanza ambapo alisema wengi waliona anazungumza mambo ambayo yanatoka hewani.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amewaagiza Naibu Waziri wa Tamisemi na Waziri wa Afya kufuatilia malalamiko ya wananchi kuhusu mtindo wa madaktari kuwaandikia dawa wagonjwa, lakini wanawapa maelekezo ya maduka ya kununua tabia aliyosema lazima ikomeshwe na tayari ameshaagiza vyombo vya ulinzi vifuatilie baadhi ya maeneo.
Katika hatua nyingine Dk Mwigulu amewaagiza wasimamizi wa miradi ya makandarasi kutoka nje ya nchi kuwa makini na kuwakumbusha wahusika kulipa mishahara na posho za vibarua kwa wakati, na inapokamilika miradi yao wasiondoke na madeni.
Waziri Mkuu amesema si jambo jema makandarasi kulipwa fedha zote, lakini wakiondoka wanaacha madeni kwa vibarua na wafanya kazi wao.
Amewahakikishia wananchi kuhusu ujenzi wa miundombinu na madaraja kwa baadhi ya maeneo ambayo yanasababisha mawasiliano kukatika na watu kushindwa kupita wakiwemo wanafunzi.
