Yanga yawaachia AS FAR kismati

USHINDI wa bao 1-0, ilioupata Yanga, Novemba 22, 2025, dhidi ya AS FAR Rabat, katika mechi ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, imeiachia turufu muhimu timu hiyo ya Morocco, kutokana na mwenendo mzuri wa kikosi hicho hadi sasa.

Katika mechi hiyo ya Kundi B Ligi ya Mabingwa Afrika, iliyopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, visiwani, Zanzibar, bao la Yanga lilifungwa na mshambuliaji, Prince Dube, dakika ya 58, ambapo kuanzia hapo kikosi hicho cha AS FAR, hakijapoteza tena kwenye michuano yote hadi leo hii.

Tangu, Novemba 22, 2025, AS FAR, ilipochapwa na Yanga bao hilo la Prince Dube, kikosi hicho kimecheza jumla ya mechi 14, za mashindano yote kuanzia Ligi ya Mabingwa Barani Afrika na Ligi Kuu ya Morocco (Botola Pro), bila ya kuonja kichapo.

Katika mechi 14, ilizocheza AS FAR, nane ni za Ligi ya Mabingwa Afrika na sita ni za Ligi Kuu ya Morocco (Botola Pro), na kati ya hizo imeshinda saba na kutoka pia sare saba, ikiwa ni turufu kwa timu hiyo tangu ilipochapwa na Yanga.

Ushindi wa AS FAR wa mabao 2-0, ilioupata juzi dhidi ya RS Berkane pia ya Morocco katika mechi ya kwanza ya hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, imeifanya timu hiyo kuendeleza rekodi ya kutopoteza tangu, Novemba 22, 2025.

Msimu huu wa 2025-2026, Yanga ilikuwa kundi B la Ligi ya Mabingwa Barani Afrika na kikosi hicho kiliishia hatua hiyo, baada ya kumaliza nafasi ya tatu na pointi nane tu, nyuma ya vinara, Al Ahly ya Misri, iliyomaliza na pointi 10.

Kwa upande wa AS FAR Rabat, ilimaliza kundi hilo ikiwa nafasi ya pili na pointi tisa, ikipishana pointi moja tu na Yanga iliyoshika ya tatu na pointi nane, huku JS Kabylie, ya Algeria ikiburuza mkiani, ikishika nafasi ya nne na pointi tatu.

AS FAR msimu uliopita iliishia hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, japo, msimu huu imefika nusu fainali na imeshinda mechi ya kwanza, ikipambana kuchukua taji hilo, baada ya kulikosa tangu mara ya mwisho ilipochukua mwaka 1985.