Dar es Salaam. Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, amefichua ukiukwaji mkubwa wa taratibu katika usimamizi wa mapato ya umma, baada ya uchunguzi wa ukaguzi kubaini kuwa viwanja 168 vyenye thamani ya Sh4.09 bilioni viliuzwa nje ya mfumo rasmi wa Tausi uliothibitishwa na halmashauri.
Amesema katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2025, sehemu ya fedha zilizopatikana kutokana na mauzo hayo ziliingizwa katika akaunti binafsi badala ya kuwasilishwa kwenye mifumo rasmi ya halmashauri.
Ripoti hiyo ya ukaguzi wa mwaka wa fedha 2024/25 iliwasilishwa bungeni Ijumaa, Aprili 10, 2026.
Katika jitihada za kupata ufafanuzi, gazeti la Mwananchi liliwatafuta kwa nyakati tofauti Ijumaa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais–Tamisemi, Profesa Riziki Shemdoe, pamoja na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Dk Rogers Shemwelekwa.
Licha ya mawasiliano hayo, simu zao hazikupokelewa, na hata baada ya kutumiwa ujumbe mfupi wa maandishi, hawakujibu hadi wakati wa kuchapishwa kwa habari hii.
CAG kwenye ripoti yake ameeleza kuwa miamala hiyo haikurekodiwa katika mfumo wa Tausi, huku pia kukiwa hakuna rejista za mwongozo zilizoidhinishwa, stakabadhi rasmi wala kumbukumbu za upatanisho, jambo linaloibua mashaka makubwa kuhusu uwazi na ufuatiliaji wa mapato hayo.
“Kati ya fedha zilizopatikana, Sh481.77 milioni ziliwekwa moja kwa moja katika akaunti binafsi za benki za watu ambao si watumishi wa halmashauri na hazikuwasilishwa kwa halmashauri,” amesema Kichere.
Aidha, CAG amebainisha kuwa Sh3.61 bilioni haikuthibitishwa kupokelewa, kutokana na madai kuwa fedha hizo zilikusanywa kwa njia ya taslimu bila kuwepo nyaraka za kuthibitisha, ushahidi wa kupelekwa benki au uthibitisho rasmi wa mapokezi.
Amesisitiza kuwa hali hiyo inaashiria udhaifu mkubwa katika mifumo ya udhibiti wa mapato, na ametaka hatua stahiki zichukuliwe ili kuimarisha uwajibikaji na kulinda rasilimali za umma.
Kwa mujibu wa CAG, hatua hiyo ni kinyume pia na viwango husika vya Uhasibu vya Sekta ya Umma (IPSAS), ambapo imesababisha athari za kifedha za Sh11.93 bilioni.
Kichere amebainisha hayo katika Ripoti Kuu ya mwaka ya ukaguzi wa Tamisemi, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa mwaka wa fedha 2024/25, iliyowasilishwa bungeni Aprili 10.
Amefafanua kuwa katika ukaguzi wa Manispaa ya Kibaha kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2025, uliibua hoja hizo za ubadhirifu wa mapato yaliyotokana na uuzaji wa viwanja 168.
“Mapato yatokanayo na miamala ya ardhi katika Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha yanapaswa kushughulikiwa kupitia mfumo wa usimamizi wa mapato wa Tausi kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa pamoja na taratibu za usimamizi wa fedha za umma.
“Kufanya miamala nje ya mfumo ulioidhinishwa kunadhoofisha uwajibikaji wa mapato na uwasilishaji sahihi wa taarifa za fedha,” ameongeza Kichere.
Wakati Sh3.61 bilioni hazikuthibitishwa kuwa zilipokelewa, kwa kuwa inadaiwa zilikusanywa kwa fedha taslimu bila nyaraka za kuthibitisha, ushahidi wa kuwekwa benki au uthibitisho rasmi wa mapokezi.
“Ukaguzi ulithibitisha kuwa miamala hiyo ni matukio halisi yaliyotokea na si matukio ya dhana au yanayoweza kutokea baadaye,” amesema.
Ameeleza kuwa dosari hiyo ilitokana na mapungufu katika mifumo ya udhibiti wa ndani wa usimamizi wa mapato ya ardhi, hususan matumizi ya lazima ya mfumo wa Tausi katika mauzo ya viwanja ambayo hayakutekelezwa ipasavyo.
Kichere amebainisha kuwa hatua hiyo imesababisha miamala kufanyika nje ya mifumo iliyoidhinishwa.
Pia, amesema mgawanyo wa majukumu kati ya upangaji wa viwanja, ukusanyaji wa mapato na urekodi wa miamala haukuwa thabiti, hali iliyowawezesha baadhi ya watu kushughulikia miamala bila uangalizi huru.
“Upatanisho wa mara kwa mara kati ya kumbukumbu za mauzo ya viwanja na mapato yaliyokusanywa haukufanyika, na usimamizi wa wasimamizi juu ya watumishi wanaoshughulikia mauzo ya viwanja haukuwa wa kutosha.
“Ubadhirifu wa Sh4.09 bilioni unawakilisha hasara kubwa ya mapato ya umma. Uhamishaji wa Sh481.77 milioni kwenda katika akaunti binafsi ni ukiukwaji wa kifedha uliothibitishwa,” amesema Kichere.
Amesema kushindwa kuthibitisha Sh3.61 bilioni kunaashiria kuwa sehemu kubwa ya mapato hayo huenda kisiweze kurejeshwa.
“Kutorekodi miamala hii katika mfumo ulioidhinishwa kumesababisha upungufu mkubwa katika mapato yaliyoripotiwa pamoja na salio husika katika taarifa za fedha,” amesema.
Kutokana na hilo, CAG amependekeza halmashauri hiyo kurejesha fedha zote zilizobadhirifiwa sambamba na kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya wote waliohusika, na kuwasilisha suala hilo kwa vyombo husika vya uchunguzi kwa hatua zaidi.
