Shughuli za kiuchumi, mawasiliano yarejea Rungwe daraja likikamilika

Mbeya. Huduma za mawasiliano na shughuli za kiuchumi zilizosimama kwa muda, zimerejea kwa wananchi wa Kijiji cha Ibungu wilayani Rungwe mkoani Mbeya baada ya kukamilika ujenzi wa daraja la mto Lubangalala.

Daraja hilo linalounganisha vijiji vya Ibungu (Mbeya) na Ileje ya mkoani Songwe lilisombwa na maporomoko yaliyosababishwa na mafuriko yaliyotokea Machi 15 mwaka huu wilayani Rungwe yaliyoua watu zaidi ya 20 na kadhaa kujeruhiwa.

Wakizungumza leo Aprili 12, 2026 wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya baadhi ya wananchi wamesema tangu kukatika daraja hilo, walishindwa kufanya shughuli zozote za kiuchumi na hakukuwa na mawasiliano na wenzao.

Emeria Haonga mkazi wa kijiji cha Ibungu amesema ilikuwa ni changamoto kupita eneo hilo kufuata huduma za kijamii ikiwamo afya, huku vyombo vya usafiri vikishindwa kutoa huduma.

Amesema mafuriko ya Machi 25 hayakuwaharibia miundombinu ya barabara na madaraja pekee, bali hata mazao shambani yalisombwa na sasa hawajui hatima yao.

Naibu waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya (wa kwanza kulia) akikagua ujenzi wa daraja la mto Lubangalala lililopp wilayani Rungwe ambalo lilikatika wakati wa mafuriko yaliyotokana na maporomoko yaliyotokea Machi 25. Picha na Sadam Sadick

“Tuipongeze Serikali kwa uharaka na hatua walizochukua kuturejeshea mawasiliano, hili daraja ndilo tegemeo kwa sisi na kijiji jirani cha Ileje, mafuriko yaliyotokea yalisomba hadi mazao shambani, hatujui tutaishije” amesema Emeria.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Efesi Mbuge amesema kijiji hicho kina vitongoji vinne na wakazi 245 ambapo daraja hilo ndilo kiunganishi.

“Tumekutwa na madhara makubwa sana kupitia mafuriko yaliyotokea, wananchi hawana mazao, tunafikiria kiangazi kikifika turudi shambani kupanda upya, kurejesha daraja hili niishukuru Serikali,” amesema na kuongeza;

“Naibu Waziri alianza kuja kuangalia madhara na leo tena karudi kuona maendeleo ya ujenzi, amani imerudi, mateso ya kubeba mizigo na watu yameisha, shughuli zinaendelea.”

Naye msimamizi wa mradi huo, Mhandisi Lubango Mihayo amesema daraja hilo limekamilika na lipo tayari kwa matumizi japokuwa kwa magari makubwa yanasubiri kukauka kwa zege, hatua itakayochukua takribani siku 14.

Amesema baada ya kuharibika daraja hilo, Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) waliwahi kufanyia kazi changamoto na katika ujenzi huo wameongeza urefu kutoka mita 12 hadi 20.

Daraja la mto Lubangalala linalounganisha Mikoa ya Mbeya na Songwe hadi nchi ya jirani ya Malawi ambalo lilikatika kufuatia mafuriko yaliyotokea Machi 25 mkoani Mbeya.

“Jumla ya gharama ni Sh474 milioni, ambapo kuna barabara za kuunganisha ambazo zenyewe zimegharimu Sh242 milioni, kwa sasa shughuli zinaendelea na magari madogo yanapita na makubwa yataanza kupita baada ya wiki mbili,” amesema Mhandisi huyo.

Akizungumza baada ya ukaguzi wa daraja hilo, Naibu Waziri, Kasekenya ametoa pole kwa wananchi waliokumbwa na matatizo ya maporomoko hayo na changamoto zilizojitokeza katika miundombinu hiyo na mali zao na waliopoteza wapendwa wao.

Amesema baada ya kukatika daraja hilo walitoa taarifa kwa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye alitoa kibali cha kufanya utaratibu wa kurejesha mawasiliano haraka iwezekanavyo na sasa huduma zimerejea upya.

“Nimshukuru Rais kwa kuwa licha ya daraja hili kuwa Rungwe, kuharibika waathirika zaidi ni wananchi wa Ileje jimboni kwangu zilipo kata nane wanaotumia njia hii.

“Daraja hili lina urefu wa zaidi ya mita 20 limejengwa haraka ndani ya siku 16, nimpongeze mkandarasi ambaye ni mzawa na kwa sasa unafanyika usanifu kwa barabara hizi kujengwa kwa lami,” amesema Mbunge huyo wa Ileje mkoani Songwe.