Kauli za wadau, ziara ya Chakwera ikifikisha siku nne

Dar es Salaam. Ziara ya Mwakilishi wa Jumuiya ya Madola, Lazarus Chakwera, nchini imefikisha siku ya nne, huku wachambuzi wa siasa wakisema inaonekana amepata imani ya wadau na pengine akakidhi matarajio ya umma.

Chakwera, Rais mstaafu wa Malawi, Novemba mwaka jana aliteuliwa na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Shirley Botchwey, kuwa mjumbe maalumu wa jumuiya hiyo atakayefanya ziara nchini.

Tayari kiongozi huyo ameshakutana na makundi mbalimbali ya viongozi wa kisiasa na Serikali na kufanya nao mazungumzo, ambayo hata hivyo yeye mwenyewe bado hakuyaweka wazi. Ziara yake hiyo inatarajiwa kukoma Aprili 16, mwaka huu.

Chakwera aliwasili nchini usiku wa Aprili 8 mwaka huu, na leo Aprili 12, 2026 ametimiza siku ya nne, ikiwa ni takriban miezi sita imepita tangu ilipotangazwa angewasili Novemba mwaka jana kwa ziara hiyo kama kiongozi wa ujumbe wa Jumuiya ya Madola.

Baada ya kupokelewa katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA), kesho yake alianza kwa kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo.

Baadaye, alikutana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Profesa Palamagamba Kabudi, kwa mazungumzo.

Kikao hicho kilifuatiwa na mikutano na vyama vya siasa, akianza na ACT Wazalendo, kisha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), vyote kupitia viongozi wao.

Kisha, Chakwera alikutana na Tume ya Rais ya Uchunguzi wa Matukio ya Kabla na Baada ya Uchaguzi wa Oktoba 29 mwaka jana.

Akizungumza baada ya kikao hicho, Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji mstaafu Othman Chande, amesema walitumia saa mbili kumweleza majukumu ya tume hiyo na hadidu za rejea pamoja na kujibu maswali ya ufafanuzi yaliyoulizwa.

“Tumemweleza juu ya majukumu ya tume na hadidu za rejea ambazo ziko wazi, ni kitu ambacho kila mtu anakijua. Pia, kujibu maswali ya ufafanuzi anayotaka kujua hasa kuhusu majukumu ya tume,” amesema.

Hata hivyo, Chakwera pia amesikika akisema kila kinachofanyika ni kwa ajili ya Tanzania na Watanzania.

Akizungumzia hilo, mchambuzi wa siasa, Dk Deus Mwapamba, amesema ziara hiyo imeonesha taswira ya ushirikiano unaotia matumaini kutoka kwa wadau mbalimbali wa kisiasa nchini.

Ameeleza kuwa kitendo cha kupata ushirikiano kutoka kwa vyama vya siasa, viongozi wa Serikali na tume kinaashiria kuwa kuna nia ya kusikilizana, jambo ambalo ni muhimu katika mazingira yenye changamoto za kisiasa.

“Vikao vya aina hiyo mara nyingi vinaweza kuwa vya heshima na kidiplomasia zaidi kuliko uhalisia wa kile kinachoendelea chini kwa chini, hivyo ni muhimu kusubiri matokeo yatakayofuata kabla ya kutoa hitimisho la mwisho,” amesema.

Kuhusu matarajio ya umma, amesema anaamini Chakwera ana nafasi ya kuwa kiungo muhimu cha mazungumzo ya kitaifa, lakini mafanikio yake yatategemea zaidi utayari wa wadau wa ndani kuyapokea na kuyatekeleza mapendekezo yatakayojitokeza.

Kwa upande wa mchambuzi wa siasa na mtafiti wa masuala ya utawala bora, Rehema Sanga, amesema ziara hiyo imekuja katika wakati ambao nchi inahitaji majadiliano ya wazi na jumuishi.

“Ushirikiano alioupata Chakwera kutoka kwa pande mbalimbali ni hatua muhimu ya kujenga mazingira ya kuaminiana, hasa kwa kuzingatia historia ya karibuni,” amesema.

Hata hivyo, ametahadharisha kuwa ushirikiano huo haupaswi kupimwa kwa kuangalia tu idadi ya mikutano au orodha ya watu aliokutana nao.