Samata aandika historia, akifunga bao la kwanza Ufaransa

Mbwana Samatta jana Jumapili, Aprili 12, 2026 amefunga bao la kwanza akiwa na jezi ya Le Havre katika mchezo wa Ligi Kuu ya Ufaransa ‘Ligue 1’ uliomalizika kwa sare ya bao 1-1.

Kwenye mechi hiyo ambayo Le Havre ilikuwa ugenini katika Uwanja wa Allianz Riviera, Samatta alifunga bao hilo katika dakika ya 41 akimalizia pasi ya Rassoul Ndiaye.

Tangu Samatta alipojiunga na Le Havre katika dirisha kubwa la usajili la majira ya kiangazi, nahodha huyo wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ alikuwa hajaifungia timu hiyo hadi alipofanya hivyo jana.

Bao hilo limekuja wiki tatu tangu Samatta alipopiga pasi ya bao katika mechi ya Ligi Kuu Ufaransa dhidi ya Paris FC waliyofungwa mabao 3-2.

Katika mechi ya jana, Samatta alifanyiwa mabadiliko katika dakika ya 87 akimpisha Stephan Zagadou.

Matokeo ya jana yameifanya Le Havre ibakie katika nafasi yake ya 14 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Ufaransa ikifikisha pointi 29.

Nice nayo imebaki katika nafasi yake ya 15 ikifikisha idadi ya pointi 28. Bao hilo la Samatta jana limemfanya sasa awe amefunga katika Ligi tano tofauti barani Ulaya.

Samatta amefunga katika Ligi Kuu England (EPL), Ligi Kuu Ubelgiji, Ligi Kuu Uturuki, Ligi Kuu Ufaransa na Ligi Kuu ya Ugiriki.