BAADA ya Mashujaa FC, kumkosa aliyekuwa beki wa kati wa kikosi cha Coastal Union, Mzenji Haroub Mohamed, katika dirisha dogo la Januari 2026, inaelezwa mabosi wa maafande hao wanapambana naye kwa ajili ya kuipata saini yake kwa msimu ujao.
Mashujaa FC ilionyesha nia ya kumuhitaji beki huyo katika dirisha dogo la Januari 2026, baada ya kuondoka kwa Abdulmalik Zakaria, aliyejiunga na timu ya Singida Black Stars, ili awe mbadala wake, japo, hesabu hizo ziligonga mwamba mwishoni.
Licha ya Mashujaa kuonyesha nia kwa nyota huyo, ila ilishindwa vita hiyo na Geita Gold inayoshiriki Ligi ya Championship msimu huu, ambayo ilimnasa na sasa anakipambania kikosi hicho ili kirejee Ligi Kuu baada ya kushuka msimu wa 2023-2024. Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata, zinaeleza mabosi wa Mashujaa bado wanaendelea kumfukuzia beki huyo, ambaye mwishoni mwa msimu huu mkataba wake na Geita Gold wa miezi sita aliousaini Januari 2026, akitokea Coastal Union, unafikia tamati.
“Tumeanza mazungumzo ya kuhakikisha tunakamilisha taratibu hizo mapema kabla ya msimu kuisha, kwa sababu ushindani kwa kipindi hicho utakuwa ni mkali zaidi, kwa sasa tunaendelea kupambana kutokana na mahitaji yetu,” kilisema chanzo hicho.
Katika dirisha dogo la Januari 2026, mbali na Mashujaa ila beki huyo alikuwa akihusishwa na kujiunga na TRA United, JKT Tanzania na KMC FC, ambazo zote zilionyesha uhitaji, japo, alichagua Geita Gold na kuzitosa timu zinazoshiriki Ligi Kuu. Nyota huyo alijiunga kwa mara ya kwanza na Coastal Union, Julai 10, 2024, akitokea Malindi SC ya visiwani, Zanzibar kwa mkataba wa miaka miwili na kwa sasa amekuwa muhimili katika kikosi cha Geita Gold, chini ya Kocha, Zubery Katwila.
Hadi sasa, Geita Gold iliyoshuka daraja msimu wa 2023-2024, ikitokea Ligi Kuu hadi Championship, kwa msimu huu inaongoza Ligi ikiwa na pointi zake 52, baada ya kikosi hicho kucheza mechi 21 na kimeshinda 16, sare nne na kupoteza moja.
