Papa Leo XIV aanza ziara Afrika leo

Dar es Salaam. Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Leo XIV, leo Aprili 13, 2026 ameanza rasmi ziara yake ya kipapa barani Afrika, ikiwa ni safari yake ya kwanza katika bara hilo tangu achaguliwe mwaka 2025 na pia ndiyo ndefu zaidi kuwahi kufanya tangu aingie madarakani.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Vatican (Vatican News), ziara hiyo ya siku 10 itakayokamilika Aprili 23, 2026, itampeleka katika nchi za Algeria, Cameroon, Angola na Equatorial Guinea.

Akizungumza na wanahabari Alhamisi, Aprili 9, 2026, Mkurugenzi wa ofisi ya habari ya Vatican, Matteo Bruni, alifafanua uzito wa ziara hiyo akisema itabeba ujumbe wa kitume na kidiplomasia.

“Ni safari ya kitume inayopitia nchi nne zenye utajiri mkubwa wa historia, tamaduni na mila, lakini pia zenye changamoto za kijamii na kisiasa, ikiwemo migogoro, uhamiaji na kuishi pamoja kwa dini tofauti,” alisema.

Aliongeza kuwa katika hotuba zake, Papa atazungumzia masuala ya amani, uhamiaji, mazingira, vijana na familia, akisisitiza kuwa ujumbe huo unalenga kuimarisha mshikamano wa kijamii na maendeleo jumuishi.

Alisema ziara hiyo pia ina mwelekeo wa kidiplomasia, ikilenga kuhimiza maridhiano, kupunguza migogoro na kusukuma ajenda ya haki ya kijamii katika mataifa hayo yanayokabiliwa na changamoto za kiuchumi na kisiasa.

Safari hiyo inaanzia nchini Algeria, ikiwa ni mara ya kwanza kwa Papa kutembelea taifa hilo lenye Waislamu wengi.

Akiwa huko, atasisitiza mazungumzo kati ya dini tofauti hasa Ukristo na Uislamu, pamoja na kushughulikia suala la uhamiaji.

Pia atatoa heshima kwa mashahidi 19 waliouawa wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe, akirejea urithi wa Mtakatifu Augustine kama ishara ya kukuza maridhiano.

Akitoka hapo, ataelekea Cameroon, ambako kwa mujibu wa Vatican, anatarajiwa kugusia masuala ya amani, mshikamano wa kijamii na maendeleo ya binadamu, hasa katika maeneo yaliyoathiriwa na migogoro ya muda mrefu.

Ziara hiyo itaendelea nchini Angola, ambapo pamoja na utajiri wa rasilimali, changamoto ya ukosefu wa usawa bado ipo.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ufaransa (RFI) Papa anatarajiwa kutumia jukwaa hilo kusisitiza umuhimu wa haki ya kijamii na kupambana na ufisadi.

Papa atahitimisha ziara yake nchini Equatorial Guinea, akilenga masuala ya elimu, utamaduni na mchango wa Kanisa katika kukuza amani, huku akitazamiwa pia kusawazisha msimamo wake katika mazingira yenye changamoto za kisiasa.

Kwa ujumla, Vatican inaeleza kuwa ziara hiyo inaonesha umuhimu unaoongezeka wa Afrika ndani ya Kanisa Katoliki duniani, hasa ikizingatiwa kuwa bara hili linachangia takribani asilimia 20 ya waumini wote.

Kwa muktadha huo, ziara ya Papa Leo XIV inatazamwa kama jukwaa muhimu la kuimarisha maadili ya amani, mshikamano na haki ya kijamii, huku pia ikifungua mjadala mpana kuhusu nafasi ya Afrika katika mustakabali wa Kanisa na dunia kwa ujumla.