Hakimu Mkazi anavyopambania haki yake mahakamani

Dodoma. Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu ya Dodoma, imempa muda wa siku 14, aliyekuwa Hakimu Mkazi Daraja la II, Benson Ngowi, kufungua maombi ya mapitio ya mahakama, ili kupinga kufutwa kazi na mhimili huo wa dola.

Uamuzi huo ambao ulipakiwa Aprili 11, 2026 katika tovuti ya TanzLII ni tovuti ya Serikali ya Tanzania inayochapisha maamuzi, sheria na kanuni bure mtandaoni, umetolewa na Jaji Abdi Kagomba wa Masjala Kuu ya Dodoma.

Hii ni wakati akitoa uamuzi wa maombi ya kibali cha kufungua mapitio ya mahakama, yaliyofunguliwa na Ngowi dhidi ya Kamati ya Maadili ya Maofisa wa Mahakama, Mtendaji Mkuu wa Mahakama na Tume ya Utumishi wa Mahakama.

Halikadhalika katika maombi hayo namba 1937 ya mwaka 2026, Ngowi alimuunganisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kama mjibu maombi wa nne.

Kulingana na mwenendo wa shauri hilo, muombaji alikuwa mwajiriwa wa mjibu maombi wa tatu, ambaye ni Tume ya Utumishi wa Mahakama kama Hakimu Mkazi Daraja la II kuanzia Februari 15,2021 kabla ya kufutwa kazi Desemba 17,2025.

Kufutwa kwake kazi kulitokana na usikilizwaji wa shauri la kinidhamu lililoendeshwa na mjibu maombi wa kwanza, ambayo ilimtia hatiani kwa makosa mawili, moja kushindwa kufuata maagizo na pili, ni la kuwa na tabia mbaya.

Hakuridhishwa na uamuzi huo, akaamua kufungua maombi ya kupatiwa kibali cha mahakama ili aweze kufungua maombi ya kufungua mapitio ya mahakama na akaomba yasikilizwe chemba, lakini wajibu maombi wakaomba nao wajibu.

Usikilizwaji wa maombi hayo ulifanyika kwa njia ya mawasilisho ya maandishi ambapo muombaji aliandaa mwenyewe nyaraka hizo,  wakati za wajibu maombi ziliandikwa na Jenipher Kaaya, wakili Mwandamizi wa Serikali.

Alivyojenga hoja ya maombi

Katika wasilisho lake la maandishi, muombaji aliegemea uamuzi wa kesi nyingine ambayo iliweka vigezo vya maombi ya aina hiyo kukubaliwa kuwa ni pamoja na muombaji awe amejenga msingi wa haja ya kesi au prima facie case.

Vigezo vingine ni kuonyesha nia ya kutosha katika kesi hiyo, kujaza maombi ya likizo ndani ya miezi sita tangu tarehe ya uamuzi, kuwepo kwa uamuzi wa kupingwa, kumaliza nafuu zilizopo na maombi yafanywe kwa nia njema.

Ngowi alijenga hoja kuwa uamuzi wa kumfuta kazi uliofanywa na mjibu maombi wa tatu ulitolewa Desemba 17,2025 na yeye akafungua maombi hayo Februari 2026, hivyo yupo ndani ya muda uliowekwa wa kufungua ndani ya miezi sita.

Kuhusu ‘prima facie case’, mwombaji aliwasilisha kwa kina makosa kadhaa anayoona kuwa yameathiri uamuzi wa mwajiri wake anaoupinga na kuhusu kuwa na masilahi, alisema anayo na maombi kwa kuwa ndiye aliyefutwa kazi.

Ngowi alisema kuhusu uwepo wa uamuzi unaopingwa, muombaji huyo alieleza uamuzi huo kupitia kiambatanisho BEN 11 na kama maombi hayo yana nia njema, alisema hilo lipo katika nafuu ambayo anakusudia kuiomba kwenye mapitio.

Katika majibu yao, walisema muombaji hajaweza kuishawishi mahakama juu ya uwepo wa msingi wa kesi kutokana na ukweli kuwa alishindwa kupata mwenendo wa shauri la kamati ya nidhamu na ripoti ya uchunguzi iliyofanywa na mwajiri.

Jaji akasema ni jambo lisilobishaniwa na pande mbili kuwa nyaraka hizo hazikuambatanishwa na muombaji katika maombi ya kuunga mkono maombi hayo.

Lakini kulingana na wajibu maombi, ili mahakama hiyo iweze kujiridhisha kwamba vigezo vyote muhimu vimetimizwa, muombaji alikuwa anawajibika kuwasilisha ushahidi zaidi nje ya barua ya kufutwa kazi, ili kuthibitisha madai yake.

Wakiegemea maamuzi ya kesi mbalimbali, wajibu maombi hao walisema ni wajibu wa mleta maombi kuwasilisha kumbukumbu zote ikiwamo uamuzi unaopingwa na kushindwa kufanya hivyo ni dosari mbaya ya kiutaratibu, kwani hiyo ndiyo inatengeneza msingi wa kufungua maombi ya mapitio ya mahakama.

Akijibu hoja hizo, muombaji alisimama katika msimamo wake wa awali na kusema hata maamuzi ya kesi zilizorejewa na wajibu maombi, hazifanani na kesi yake.

Kuhusu kutoambatanishwa kwa ripoti ya uchunguzi na mwenendo wa shauri la kinidhamu, mwombaji alishikilia msimamo kuwa hati hizo ni muhimu katika ufunguaji wa maombi ya kibali cha kufungua maombi hayo lakini si za lazima.

Kulingana na muombaji, alisema ameibua hoja ambazo hazijajibiwa na wahojiwa na kurejea kiapo chake kwamba aliomba nyaraka hizo kutoka kwa mwajiri pasipo mafanikio na kwamba atazitumia wakati atakapofungua maombi ya mapitio.

Baada ya kupitia hoja hizo, Jaji Kagomba alisema hoja inayopaswa kuamuliwa ni iwapo muombaji amekidhi masharti ya kisheria yanayoishawishi mahakama hiyo kuyakubali maombi ya kibali cha kufungua maombi ya mapitio ya mahakama.

Jaji alisema katika mawasilisho ya pande mbili, ni jambo lililo wazi kwake kwamba maombi hayo yasingepingwa na wajibu maombi kama muombaji angeambatanisha ripoti ya uchunguzi na mwenendo wa kamati ya nidhamu.

“Kikubwa, pingamizi la wajibu maombi ni kwamba kwa kuwa mwombaji ana nia ya kupinga kusitishwa ajira kwa makosa, barua ya kuachishwa kazi peke yake haifai kuwa mwanzo kwa sababu hajabeba makosa hayo yanayolalamikiwa”

Jaji akaongeza:- “wajibu maombi wanaona kwamba, kabla ya kuwasilisha ombi hili, mwombaji alipaswa kukusanya, kutoka kwa mwajiri, ripoti ya uchunguzi na rekodi za mwenendo na kuziambatanisha ili kuwezesha mahakama hii kuamua ombi hili.”

“Kwamba, kwa hali ilivyo, mahakama hii haiwezi kuamua kihalali kama kuna ukiukwaji huo wa kibali cha kuendelea na mapitio ya mahakama,”alisema Jaji.

“Kwa kuzingatia mipaka (confines) ya hoja ya wajibu maombi katika shauri hili, basi suala mahsusi litakaloamuliwa katika suala hili ni iwapo mwombaji ameibua hoja inayobishaniwa ili kibali cha kufungua mapitio ya mahakama kitolewe”

Jaji alirejea kanuni ya 8(1)(a) ya GN namba 324 iliyotangazwa 2014 ambayo inasema pale kibali cha kufungua mapitio ya mahakama kinapokuwa kimetolewa, muombaji atawasilisha kiapo na maelezo kwa nini mapitio yanayoombwa.

Kulingana na Jaji, kile kitakachoibuliwa hatua ya maombi ya kibali, ndio yatapenya pia kwenye maombi ya mapitio ya mahakama hivyo kama kuna nyaraka haikuingia katika hatua ya maombi ya kibali, haiwezi kuingia katika maombi ya mapitio.

“Hata hivyo, ni maoni yangu kuwa ukiukwaji wa taratibu unaohusu shauri la kinidhamu na ripoti ya uchunguzi, kama upo, sio yote ambayo mwombaji analalamikia. Kuna masuala mengine yanayobishaniwa yaliyotolewa na mwombaji yenye uwezo wa kuendeleza ombi hili la kibali cha kufungua maombi,”alisema Jaji.

Jaji aliyataja masuala hayo kuwa ni pamoja na malalamiko ya mwombaji kuwa mjibu maombi wa kwanza alishindwa  kuzingatia nafasi ya sheria kwa kuendelea kurekebisha hati ya mashtaka mara kadhaa, si wakati wa kusikilizwa, na si ndani ya siku 30 tangu tarehe ambayo shtaka la kwanza lilikabidhiwa kwa mwombaji.

Pia alishindwa kuzingatia kwamba makosa yote ambayo alitiwa nayo hatiani hayapelekei adhabu kwani kosa la kwanza lilistahili kupewa onyo wakati kosa la pili halikuhusisha kitendo chochote au jaribio la kosa la kulawiti (unnatural offence).

Mbali na hilo, mwombaji amedai kuwa hakupewa ripoti ya upelelezi na hati ya mashtaka iliyopelekea kukutwa na hatia na kuhukumiwa, hivyo ni maoni yake kuwa dai hili pia linatilia shaka usahihi wa maamuzi ya kumfuta kazi ya uhakimu.

“Kwa kuwa, kuna masuala ya ubishani yanajitokeza nje ya ripoti ya uchunguzi na taratibu za kinidhamu na kwa kuwa mwombaji ana masilahi katika suala hili, amefungua maombi ndani ya muda wa miezi sita, hana nafuu zaidi na hajawasilisha maombi haya kwa nia mbaya, ninaamua kuwa mwombaji amekidhi vigezo vyote vya kumpa kibali cha kufungua mapitio ya mahakama,”alisema Jaji.

Ni kwa msingi huo, Jaji alimpa siku 14 kuanzia tarehe ya uamuzi huo, kufungua maombi ya mapitio ya mahakama kupinga kufutwa kazi.