Polisi Zanzibar yatoa kauli kifo cha Mmarekani Ashlee Jenae

Zanzibar. Polisi visiwani Zanzibar limezungumzia kifo cha mwanaharakati wa mitandao ya kijamii kutoka Miami, nchini Marekani, Ashly Robinson (31), maarufu mtandaoni Ashlee Jenae.

Taarifa ya Polisi, inakuja wakati ambao kumekuwa na mijadala katika majukwaa ya kimataifa ya mitandao ya kijamii kuhusu kifo cha mwanaharakati huyo, baadhi wakiibua hisia kali.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja, Benedict Mapujira, ameiambia Mwananchi, leo Jumatatu, Aprili 13, 2026 uchunguzi wa awali unaonesha kifo hicho ni cha kujiua.

Amesema tukio hilo lilitokea Alhamisi, Aprili 9, 2026, mwanamke huyo anadaiwa kujinyonga kwa kutumia kipande cha nguo kutoka katika vazi lake, ndani ya kabati la chumbani.

Ameeleza mwanaharakati huyo, alikwenda visiwani Zanzibar na mpenzi wake kwa ajili ya furaha, lakini baadaye likatokea tukio hilo la kusikitisha.

Kwa mujibu wa maelezo ya polisi, Ashlee alikuwa akiishi hotelini pamoja na mchumba wake, lakini wawili hao walidaiwa kuwa na hali ya kutoelewana.

Hali hiyo, kwa mujibu wa taarifa ya polisi, ikasababisha uongozi wa hoteli kuingilia kati na kuwatengea vyumba tofauti ili kupunguza mvutano uliokuwa umejitokeza.

“Kama ilivyoripotiwa, kulikuwa na kutoelewana na baadaye uongozi wa hoteli uliamua kuwatenganisha vyumba, hivyo mwanamke akawa na chumba chake na mwanaume chake,” amesema Kamanda Mapujira.

Amesema taarifa ya tukio hilo iliripotiwa Kituo cha Polisi Nungwi baada ya wafanyakazi wa hoteli kutoa tahadhari wakihofia kuwa mgeni huyo alikuwa katika hatari ya kujiua, jambo linaloashiria kuwa huenda kulikuwa na dalili za awali zilizotia shaka kabla ya tukio kutokea.

“Mwanamke huyo alikuwa na mwenzake, mtalii aliyekuwa amekuja visiwani hapa kwa ajili ya utalii. Alikuwa bado hai wakati taarifa ilipofikishwa polisi. Aliokolewa na kupelekwa hospitalini, hata hivyo alifariki dunia siku iliyofuata (Ijumaa, Aprili 10),” amesema.

Mamlaka zimethibitisha, mwili wa marehemu bado upo nchini Tanzania ukisubiri uchunguzi zaidi wa kitabibu, ikiwa ni utaratibu wa kawaida unaolenga kubaini kwa uhakika chanzo cha kifo kabla ya maandalizi ya kuusafirisha kwenda Marekani kukamilishwa.

Alipoulizwa kuhusu hatua zozote za kisheria dhidi ya mchumba wake, Kamanda Mapujira amesisitiza hakuna msingi wa kumshikilia kwa mujibu wa mazingira ya sasa ya tukio hilo.

“Hatuwezi kuchukua hatua za kisheria au kumzuia chini ya mazingira haya,” amesema, akisisitiza msimamo wa polisi wakati mijadala na tuhuma ikiendelea kushamiri mitandaoni.

Kwa mujibu wa taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii, Ashly alisafiri kuja Zanzibar kusherehekea siku yake ya kuzaliwa Aprili 5,mwaka huu safari ambayo mwanzoni ilionekana kuwa ya furaha, iliyojaa kumbukumbu nzuri na nyakati za kipekee kati yake na mwenza wake.

Katika safari hiyo, mchumba wake, anayetajwa katika mijadala ya mtandaoni kama McCann, anadaiwa kumposa wakati wa matembezi ya wanyamapori, tukio ambalo familia yake baadaye walilielezea kuwa la kipekee.

Wawili hao walikuwa wamefikia katika hoteli ya Zuri Zanzibar wakati tukio hilo linatokea.

Katika taarifa ya pamoja, familia za Robinson na Endres zilichora picha ya furaha iliyokuwepo kabla ya tukio hilo na namna ilivyogeuka ghafla kuwa huzuni isiyoelezeka.

“Muda mfupi alikuwa akisherehekea upendo na maisha kwa namna yake ya kipekee, na ghafla akawa hayupo tena. Tukio la ghafla, maswali yasiyo na majibu na umbali kutoka nyumbani, vimeifanya huzuni hii kuwa nzito zaidi kwa familia yetu,” ilieleza familia katika taarifa yao.

Taarifa iliyochapishwa na Savannah Britt, rafiki wa karibu wa marehemu, alionesha wasiwasi kuhusu kile alichokiita ukimya au ucheleweshaji wa taarifa rasmi katika hatua za awali za tukio hilo.

“Ni jambo la wasiwasi kwamba mwanamke wa Marekani amefariki nje ya nchi siku kadhaa zilizopita na kabla ya ujumbe wangu wa kwanza, hakukuwa na taarifa yoyote kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Serikali ya Tanzania, au vyombo vya habari vya ndani,” aliandika.

Familia zimethibitisha kuwa, zinaendelea kushirikiana na mamlaka za Zanzibar katika uchunguzi unaoendelea, huku zikiwataka wananchi na watumiaji wa mitandao kuwa makini na kuepuka kusambaza taarifa ambazo hazijathibitishwa rasmi.

“Ashly alipendwa sana. Alikuwa mchangamfu, mwenye furaha ya maisha na alikuwa na mengi mazuri mbele yake,” ilieleza taarifa hiyo.

Licha ya msimamo uliotolewa na polisi, mjadala mtandaoni umeendelea kushika kasi, huku baadhi ya watumiaji wa majukwaa kama Reddit na Threads wakitoa nadharia mbadala kuhusu mazingira ya kifo cha Ashly.

Baadhi ya machapisho yamedai kuwa huenda mchumba wake alihusika katika kifo hicho, yakidai kuwa tukio hilo lingeweza kupangwa kuonekana kama kujiua, madai ambayo hayajathibitishwa na hayajaungwa mkono na mamlaka hadi sasa.

Wengine wamehoji muda wa tukio hilo, likitokea siku chache tu baada ya sherehe ya kuzaliwa na tukio la posa, wakiona mlolongo huo wa matukio kuwa wa kutatanisha na unaoibua maswali zaidi.

“Mwanamke aliyeposwa hivi karibuni hawezi kujinyonga siku chache baadaye,” ilisomeka nukuu moja ya ujumbe uliochapishwa Instagram.

Kupitia majukwaa ya X, Instagram, Reddit, Threads na mengineyo, wito wa kufanyika kwa uchunguzi wa kina na wa uwazi umeendelea kuongezeka, huku watumiaji wakitaka ukweli kamili ujulikane na mamlaka kuhakikisha hakuna jambo linalopuuzwa katika kufichua kilichotokea.

Akaunti ya Instagram ya Ashly imefurikwa na salamu za rambirambi, wafuasi wake wamekuwa wakichanganya ujumbe wa pole na madai ya kutaka haki ipatikane, hali inayoonesha mchanganyiko wa huzuni na kiu ya majibu.

Familia yake pia, imeomba subira wakati uchunguzi ukiendelea, ikisisitiza umuhimu wa taarifa rasmi katika kipindi hiki chenye hisia kali na sintofahamu.

Uchunguzi wa tukio hilo bado unaendelea, huku mamlaka zikiwataka wananchi kuepuka kutoa taarifa potofu au kusambaza taarifa zisizo na uhakika, wakati juhudi za kubaini kwa kina mazingira yote ya kifo hicho zikiendelea.