MCT yaibua vigezo vipya EJAT 2026, matokeo ya stori kuwa kipimo kikuu

Dar es Salaam. Baraza la Habari Tanzania (MCT) limeibua sura mpya ya ushindani katika Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT) 2026 kwa kutangaza vigezo vipya vinavyoweka mkazo mkubwa kwenye matokeo ya stori kwa jamii, ubora wa uandishi na uzingatiaji wa misingi ya kitaaluma.

Hatua hiyo imekuja sambamba na uzinduzi wa mfumo mpya wa kidijitali wa kuchakata kazi za washiriki, ukiwa ni mabadiliko makubwa katika historia ya tuzo hizo zinazowakutanisha wanahabari kutoka vyombo mbalimbali nchini.

Akitoa neno la ufunguzi wakati wa utambulisho wa majaji, leo Jumatatu, Aprili 13, 2026, Katibu Mtendaji wa MCT, Ernest Sungura, amesema maandalizi ya mfumo huo yamechukua takribani miaka miwili ya utafiti na yameleta matokeo chanya katika kuboresha utendaji.

“Kwa mara ya kwanza, MCT tunachakata shindano hili kwa kutumia mfumo tofauti na awali. Lengo ni kuongeza uwazi, ufanisi na haki kwa washiriki wote,” amesema Sungura.

Amebainisha jumla ya waandishi wa habari wapatao 600 pamoja na majaji 12 wameingia kwenye mfumo huo, wakitarajiwa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa mwaka huu.

Katika kusisitiza mwelekeo mpya wa ushindani, Sungura amesema majaji hawataangalia ubora wa uandishi pekee, bali pia athari halisi ya stori kwa jamii.

“Hatutaishia kwenye mfumo tu, tutakwenda mbali zaidi hadi kuhakiki matokeo ya stori katika maeneo husika. Stori yoyote isiyo na matokeo haitatangazwa kushinda tuzo,” amesema.

Ameongeza vigezo vingine vitahusisha ubora wa maudhui, uandishi unaozingatia kanuni za taaluma na maadili ya uandishi wa habari.

Kwa upande wa majaji, Sungura amesema wamepatikana kupitia mchakato makini uliolenga kupata wataalamu wabobezi kutoka maeneo mbalimbali ya tasnia hiyo.

“Majaji tulio nao ni magwiji waliobobea katika TV, redio na magazeti, na tuna imani watasimamia mchakato huu kwa haki na weledi mkubwa,” amesema.

Majaji hao ni Jesse Kwayu, Joyce Shebe, Beatrice Bandawe, Rashid Kejo, Dk Wilbert Mkoko, Hassan Mhelela, Absalom Kibanda, Neville Meena, Mwanzo Milinga, Aisha Dache, Sauli Juliadi na Shufaa Said Hassan.

Akizungumza wakati wa kuwaapisha majaji hao, Wakili Ally Kileo amewataka kuzingatia sheria, maadili na kuepuka upendeleo katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Ni matumaini yetu kuwa mtasimamia kwa haki na weledi ili kuwapata washindi bora wa tuzo hizi,” amesema.

Baadhi ya majaji wameeleza dhamira yao ya kuhakikisha mchakato huo unakuwa wa haki na wenye tija kwa jamii.

Dk Wilbert Mkoko amesema watajikita katika kupima mchango wa stori kwa jamii.

“Tutazingatia namna stori ilivyoleta mabadiliko chanya katika jamii iliyokusudiwa,” amesema.

Kwa upande wake, Neville Meena, aliyewahi kuwa mshindi wa jumla mwaka 2011, amesema uzoefu wake unaonesha tuzo hizo ni chachu ya mafanikio kwa wanahabari.

“Nilishiriki na kushinda katika maeneo ya teknolojia na utawala bora, na ushindi huo ulinifungulia milango mingi kitaaluma hadi leo nimetunukiwa jukumu la kuwa jaji.

“Teknolojia ya Akili Unde (AI) ni muhimu katika uandishi wa habari wa kisasa. Waandishi wanapaswa kuitumia kwa ufanisi, lakini wakumbuke kuwa ubunifu na uamuzi wa mwisho unapaswa kubaki kwa binadamu,” amesema.

Naye Joyce Shebe amesema mashindano hayo yamekuwa na mchango kubwa katika kukuza viwango vya uandishi nchini.

“Tukisimamia kwa weledi, tutapata washindi bora na kusaidia jamii kupata taarifa sahihi na zenye tija,” amesema.

Tuzo za EJAT 2026 zinatarajiwa kutolewa Mei 29, 2026 baada ya majaji kukamilisha mchakato wa tathmini, huku wadau wakisubiri kuona athari za vigezo vipya katika ushindani huo na washindi watakaopatikana.