MCHENGERWA AONGOZA TIMU YA TANZANIA MKUTANO WA 59 WA KAMISHENI YA IDADI YA WATU NA MAENDELEO NCHINI MAREKANI

Na John Mapepele, New York -Marekani  

Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa ameongoza timu ya Tanzania katika Mkutano wa 59 wa Kamisheni ya Idadi ya Watu na Maendeleo unaofanyika New York Nchini Marekani.

Mhe. Mchengerwa amesema Mkutano huo ambao umeanza leo Aprili 13,2026 na utaendelea  hadi Aprili 17, 2026 unalenga kuimarisha uhusiano kati ya idadi ya watu, teknolojia, utafiti na maendeleo endelevu, pamoja na kusaidia nchi kupanga sera bora za maendeleo kulingana na takwimu na ubunifu wa kiteknolojia. 

Mhe.Mchengerwa amefafanua kuwa mambo mengine muhimu yatakayojadiliwa wakati wa vikao hivyo ni pamoja na Teknolojia katika afya ya uzazi na afya ya jamii ikiwemo teknolojia mpya za uzazi wa mpango (contraception), Utafiti katika “reproductive health”, matumizi ya “telemedicine na digital health platforms” pamoja na upatikanaji wa huduma za afya kwa vijana na wanawake.

Aidha, Mhe. Mchengerwa ambaye pia ameambatana na Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia eneo la Madawa na Vifaa Tiba, Bwana Emmanauel Tayari anayetarajia  kutoa mada  mahususi kwenye mkutano huo kuhusu  Tanzania.

Sanjari na vikao hivyo, Mhe. Mchengerwa anatarajia pia kuwa na vikao kadhaa na wakuu mbalimbali wa mashirika  ya Afya, na mabalozi  wa nchi mbalimbali kuzungumzia  masuala  mbalimbali ya kimkakati katika sekta  ya Afya.

Mkutano huu unahusisha zaidi ya nchi 193 kutoka sehemu mbalimbali duniani pamoja  na mashiriki  yote  makubwa yanayojishuhulisha na  masuala ya afya.