Iringa. Mkoa wa Iringa umepanga kufanya maonyesho ya kilimo kuanzia Julai 13 hadi 19, 2026 katika viwanja vya Kihesa Kilolo ili kuinua sekta ya kilimo kwa kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara, pamoja na kuwasaidia wakulima kupata mbinu bora zaidi za uzalishaji zinazokidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi.
Maonyesho hayo yanatajwa kuwa jukwaa muhimu litakalowawezesha wakulima kuongeza tija katika shughuli zao kwa kutumia teknolojia za kisasa, sambamba na kupata fursa za masoko na maeneo ya uwekezaji, hali inayotarajiwa kubadilisha maisha ya wakulima wengi mkoani humo na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Akizungumza wakati wa kufungua kikao cha kamati ya maandalizi katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk Bahati Golyama, akimwakilisha Katibu Tawala Msaidizi wa Uchumi na Sekta za Uzalishaji, amesema maandalizi yanaendelea vizuri na Serikali imejipanga kuhakikisha maonyesho hayo yanakuwa ya mafanikio makubwa.
Dk Golyama ameeleza kuwa maonyesho hayo yataleta pamoja wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo, wakiwemo wakulima, wafugaji, wavuvi, watafiti na wawekezaji, jambo litakalosaidia kubadilishana uzoefu na maarifa kwa vitendo.
“Taasisi mbalimbali za kilimo, teknolojia ya mbegu, pamoja na taasisi za utafiti wa mazao, mifugo na uvuvi zitashiriki kikamilifu katika kuonyesha ubunifu wao, hatua ambayo itawasaidia wakulima kuona kwa vitendo teknolojia zinazoweza kuboresha uzalishaji wao,” amesema Dk Golyama.
Katika maonyesho hayo, wakulima watapata nafasi ya kujifunza matumizi ya teknolojia za kisasa zinazoweza kusaidia kuongeza mavuno na kupunguza gharama za uzalishaji, ikiwa ni pamoja na matumizi ya mbegu bora, mbinu za umwagiliaji na udhibiti wa magonjwa ya mazao.
Aidha, washiriki watapata fursa ya kuonyesha ubunifu wao katika sekta ya kilimo na ufugaji, huku wakishindanishwa kulingana na vigezo vitakavyowekwa na taasisi mbalimbali, hali inayotarajiwa kuongeza ari ya ubunifu na ushindani chanya miongoni mwa wakulima.
Wananchi wa Mkoa wa Iringa pia watapata fursa ya kujionea maendeleo ya sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi na jinsi ambavyo imekuwa ikichangia kukuza kipato cha mkulima mmoja mmoja pamoja na uchumi wa taifa kwa ujumla.
Mkulima wa mazao ya mahindi kutoka Wilaya ya Kilolo, Juma Mligo, amesema maonyesho hayo yanakuja wakati mwafaka kwa wakulima wanaohitaji kubadilisha mbinu zao za uzalishaji ili kukabiliana na changamoto za kilimo cha kisasa.
“Kwa sasa tunakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwemo mabadiliko ya tabianchi, hivyo kupitia maonyesho haya tunatarajia kupata elimu ya teknolojia mpya ambazo zitatusaidia kuongeza mavuno na kukabiliana na hali hiyo,” amesema Mligo.
Kwa upande wake, mkulima wa mbogamboga kutoka Mafinga, Rehema Mwasilwa, amesema maonyesho hayo yatasaidia katika kuwatafutia wakulima masoko ya uhakika, hasa kwa mazao yanayoharibika haraka.
“Tunazalisha lakini wakati mwingine tunakosa soko la uhakika, hivyo kupitia maonesho haya tunaamini tutapata fursa ya kukutana na wanunuzi wakubwa na kuingia mikataba ya mauzo,” amesema Mwasilwa.
Naye mwakilishi wa taasisi ya utafiti wa kilimo mkoani Iringa, Rayan Ngala, amesema maonyesho hayo yatasaidia kuunganisha tafiti zinazofanywa na taasisi na matumizi halisi kwa wakulima mashambani.
“Tunafanya tafiti nyingi lakini changamoto imekuwa ni kuwafikishia wakulima, hivyo maonyesho haya ni fursa ya kuonyesha mbegu bora na teknolojia zinazoweza kutumika moja kwa moja kuongeza tija,” amesema.
Ofisa kutoka taasisi ya maendeleo ya mifugo amesema wafugaji nao watanufaika kwa kupata elimu ya kisasa kuhusu ufugaji wenye tija na unaozingatia mahitaji ya soko.
“Tutatoa elimu kuhusu lishe bora ya mifugo, udhibiti wa magonjwa na mbinu za kuongeza uzalishaji wa maziwa na nyama ili wafugaji waweze kuongeza kipato chao,” amesema.
