ULEGA AIBANA TANROADS, ATOA SIKU 14 MKANDARASI BARABARA YA KISARAWE

******

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ameipa siku 14 Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) kukamilisha taratibu zote za kisheria za manunuzi, ikiwemo kumpata mkandarasi, ili kuruhusu kuanza kwa ujenzi wa barabara ya Kisarawe hadi Maneromango.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Masaki, Wilayani Kisarawe Mkoani Pwani, Ulega alisema Serikali imelenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma muhimu za kijamii ikiwemo miundombinu, elimu, afya, na kilimo, hatua itakayochochea ukuaji wa uchumi.

Alisisitiza kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kutekeleza miradi ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa barabara, ili wananchi wanufaike kikamilifu na fursa zilizopo.

“Wana Masaki, kazi yangu leo ni moja tu—kuielekeza TANROADS kukamilisha taratibu zote za kitaalamu ili ujenzi uanze. Baada ya wiki mbili, nataka kujua ni mkandarasi gani amepatikana na yuko tayari kuanza kazi,” alisema Ulega.

Aidha, Waziri huyo amewaagiza mameneja wa TANROADS na TARURA Mkoa wa Pwani kuweka utaratibu maalum wa utekelezaji wa miradi bila kukiuka sheria na taratibu, akisisitiza kuwa uwajibikaji wao utajenga imani kwa wananchi.

Aliongeza kuwa kuna umuhimu wa kuweka mikakati endelevu ya miundombinu, ikiwemo uwekaji wa taa za barabarani mara baada ya ujenzi kukamilika ili kuchochea shughuli za kiuchumi hata nyakati za usiku.

Katika hatua nyingine, Ulega amewaelekeza Mameneja wa TANROADS na TARURA kuandaa mpango kazi wa haraka wa ukarabati wa barabara zote zilizoharibiwa na mvua ili zirejee katika hali yake ya kawaida.

Akijibu ombi la Mbunge wa Jimbo la Kisarawe, Dkt. Selemani Jafo, kuhusu barabara ya Dondwe–Lukwali hadi Njia Nne kurekebishwa, Waziri Ulega alielekeza wataalamu kufika eneo hilo mara moja na kuanza kazi za matengenezo bila kuchelewa.