CMSA yahamasisha Sukuk kama mbadala fedha za maendeleo

Dar es Salaam. Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) imezitaka taasisi mbalimbali kutumia mbinu mbadala za kupata fedha kwa ajili ya shughuli za maendeleo na kuchochea ukuaji jumuishi.

Wito huo umetolewa Jumatano, Aprili 15, 2026 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Usimamizi na Uchunguzi wa CMSA, Exaud Julius wakati wa uzinduzi wa Mapato Sukuk, bidhaa mpya inayotolewa na Benki ya Biashara ya Kenya (KCB).

Akizungumza kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa CMSA, Nicodemus Mkama, Julius amesema KCB imefanya vizuri katika Sukuk iliyopita, hivyo ameziasa taasisi nyingine kuiga mfano wa benki hiyo katika kubuni njia mbadala za kupata fedha.

“Napenda kuziasa taasisi nyingine za ndani na nje ya sekta hii, kutumia mbinu nyingine mbadala za kupata fedha za maendeleo kama vile Sukuk.

“Njia hizo zimethibitishwa kuwa na ufanisi katika kukusanya mitaji, kusaidia maendeleo ya miundombinu na kukuza ukuaji jumuishi sambamba kupitia wigo mpana wa uwekezaji,” amesema.

Amewahimiza wawekezaji kushiriki katika toleo hilo la Mapato Sukuk kwani hauwakilishi tu fursa nzuri ya uwekezaji, bali pia nafasi ya kuchangia maendeleo na uchumi wa Tanzania kupitia chombo cha uwekezaji kinachozingatia misingi ya sharia.

Ameongeza bidhaa kama hizo zinapewa fursa na pia wawekezaji wanapewa anuai ili waweze kuwekeza

Amesema mauzo ya hati fungani hiyo yamekidhi matakwa ya kisheria, kanuni na miongozo ya Sukuk, hivyo ameipongeza KCB kwa kuwa kiongozi katika eneo hilo tangu walipoanza na Fursa Sukuk mwaka 2022.

Amesema katika miaka mitatu iliyo CMSA imeboresha mazingira ya uwekezaji kwenye masoko ya mitaji kwani imekuwa mstari wa mbele katika kukuza bunifu na kuunda mazingira wezeshi katika uwekezaji.

“CMSA imewezesha kutolewa kwa bidhaa mpya na wezeshi na kuiweka katika ramani ya masoko yanayotoa bidhaa bunifu ulimwenguni, yanayovutia wawekezaji wa ndani na nje,” ameeleza.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Huduma za Kibenki za Kiislamu, Amour Muro amesema Mapato Sukuk ni uwekezaji wa miaka mitatu unaozingatia sharia za Kiislamu na kima cha chini cha uwekezaji huo ni Sh500,000 ambapo ataweza kupata faida halali ya asilimia 11 kwa mwaka ambayo italipwa kila baada ya miezi mitatu.

“Faida ambayo inalipwa haikatwi kodi, yaani kodi ya zuio (Withholding Tax) na mwekezaji, pia, anaweza kuuza hiyo Sukuk yake ndani ya siku 30 baada ya mauzo ya awali ambayo yanafanyika kuanzia leo hadi Mei 14,” amesema Muro.

Amewaalika Watanzania wote wa ndani na nje ya nchi kwenda kuwekeza kwenye Mapato Sukuk na watakuwa tayari kuwapokea wawekezaji wote wenye kiasi chochote kuanzia Sh500,000.