Chuo cha Usafiri wa Anga (CATC) kwa niaba ya Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO) kimezindua rasmi mafunzo ya Vihatarishi katika Usafiri wa Anga (Risk Management Course) tarehe 20 Aprili 2026 jijini Dar es Salaam. Mafunzo haya ya siku tano yanawakutanisha washiriki 20 kutoka Tanzania, Uganda na Eswatini wakiwawakilisha mamlaka za viwanja vya ndege na mashirika ya ndege.
Lengo la mafunzo haya ni kuwajengea washiriki uwezo wa kutambua, kuchambua na kudhibiti vihatarishi vya kiusalama katika sekta ya usafiri wa anga, sambamba na kuimarisha utekelezaji wa viwango vya kimataifa vya usalama na kukuza ushirikiano wa kikanda.
Akizungumza wakati wa ufunguzi, Mkuu wa Chuo, Bw. Aristid Kanje, alisisitiza umuhimu wa mafunzo hayo katika kuimarisha usalama wa anga kikanda, akisema:
“ICAO imeweka viwango, sisi tunatekeleza. Mafunzo haya ya Vihatarishi katika Usafiri wa Anga (Risk Management Course) ni hatua muhimu katika kujenga ukanda wa anga unaotegemewa.”
Kwa upande wake, Mkufunzi wa CATC, Bi. Christine Bugoya, alielezea umuhimu wa mafunzo hayo kwa kina, akibainisha kuwa yatawaongezea washiriki mbinu za kitaalamu za usimamizi wa vihatarishi pamoja na kuboresha kwa mapana ushirikiano wa kiusalama baina ya nchi shiriki, hali itakayochangia kubadilishana uzoefu na kuimarisha mifumo ya usalama wa anga.
Kupitia mafunzo haya, Chuo cha Usafiri wa Anga (CATC) kinaendelea kuonesha dhamira yake ya kutoa mafunzo yenye viwango vya kimataifa na kuchangia kikamilifu katika kuimarisha usalama, ufanisi na maendeleo endelevu ya sekta ya usafiri wa anga kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO).
Mkuu wa Chuo cha Usafiri wa Anga (CATC), Aristid Kanje akifungua mafunzo ya Vihatarishi katika Usafiri wa Anga (Risk Management Course) yaliyoanza tarehe 20 Aprili 2026 katika chuo hicho jijini Dar es Salaam.

