Kila siku, katika miji na vijiji vyetu, tunaona watafiti wakizunguka kama “vipepeo” wakiingia kwenye shule, kwenye kliniki, kwenye vijiji, wakiuliza maswali, kuhesabu takwimu, na kukusanya maelezo mbalimbali. Wanapigana vikumbo na watu katika jamii wakijaribu kupata taarifa za utafiti, wakizungumza na wazazi, walimu, vijana, na wazee, wakijitahidi kuelewa changamoto, mahitaji, na mienendo ya jamii.
Lakini cha ajabu, mara nyingi tunapoangalia nyuma ya kazi yao, matokeo hayo hayafikii kabisa kwa wahusika.
Watafiti huiandikia ripoti, kupeleka kwa wafadhili au kwa ajili ya kupanda ngazi za kitaaluma, na matokeo yake yanajaa katika mashubaka ya maktaba. Lakini kwa kweli, mara nyingi waliohojiwa hawajui chochote.
Mfano dhahiri ni pale mtu anapofanya utafiti kuhusu sababu na athari za mimba za utotoni katika wilaya fulani. Mtafiti anaingia vijijini, akiuliza vijana, wazazi, walimu na anakusanya takwimu na maelezo ya kina.
Anapomaliza, taarifa zote zinapangwa kwa uangalifu, kuandikwa kwa umakini, na kuwasilishwa kwa mfadhili au ofisi ya kitaaluma. Lakini jamii yenyewe, ambayo imetoa ushahidi wa moja kwa moja, haiwezi kupata ripoti hiyo hata kwa nakala moja.
Kwa baadhi ya wilaya, hata maktaba ya wilaya haijui chochote kuhusu utafiti huo. Hii ni dhahiri kuwa kuna makosa makubwa ya maadili ya kitafiti na kwa hakika yanaathiri moja kwa moja dhamira ya utafiti.
Ni jambo la kushangaza jinsi kazi nyingi za kitafiti zinavyopotea katika historia ya jamii. Tunaona watafiti wakipata fedha za ufadhili, wanapanda madaraja ya kitaaluma, lakini jamii zinazotoa taarifa hazina faida yoyote.
Hii ni sawa na mtu kuandika historia ya kijiji kwa kumuuliza mtu wa kijiji, kisha kutoonyesha historia hiyo kwa wenyeji. Hali hii inawakilisha ukosefu wa maadili ya kijamii katika utafiti, kwani utafiti unaanza na jamii na unapaswa kumalizika kwa jamii.
Zaidi, kuchukua takwimu na kuandika ripoti bila mrejesho ni njia ya kupoteza maana ya utafiti. Utafiti haupaswi kuwa lengo la kupandisha hadhi ya kitaaluma tu.
Kwa kweli, malengo ya msingi ya utafiti ni kuboresha ustawi wa jamii, kusaidia jamii kuelewa matatizo yake, na kuunda suluhisho zinazofaa.
Wakati ripoti zinaishia katika maktaba, tasnifu, au mashirika ya wafadhili, tunaharibu chachu ya maendeleo ya jamii.
Wenyeji wanapata vichache, au hakuna chochote, wakati watafiti wanasherehekea mafanikio ya kitaaluma au wanapata fedha.
Kumbuka kwamba utafiti wa kijamii ni kazi ya mawasiliano. Watafiti wanapaswa kuwa madereva wa mabadiliko.
Hii inamaanisha kwa mfano baada ya mtu kuchunguza sababu na athari za mimba za utotoni, anapaswa kurudisha matokeo kwa jamii: kuwasilisha matokeo kwa viongozi wa kijiji, mashirika ya kijamii, shule, na hata vyombo vya habari vya ndani.
Jamii lazima itambue, kuelewa, na kutumia matokeo ya utafiti katika uamuzi wao wa kila siku.
Hali mbaya zaidi ni kwamba, mara nyingi hata maktaba ya wilaya au mkoa haijui utafiti huo umefanyika. Matokeo haya, ambayo yangeweza kuongoza sera bora, kuimarisha huduma za afya, au kuboresha elimu, yanaishia kuwa mafaili yasiyo na thamani kwa jamii.
Mfano mwingine ni pale utafiti unafanyika kuhusu ushirikishaji wa wanawake katika kilimo au biashara za kijamii. Watafiti huchunguza changamoto, kutoa ripoti nzuri, lakini wanawake hao hawapati hata elimu ya matokeo, na hivyo hawana nafasi ya kuboresha hali zao kutokana na taarifa zao wenyewe.
Utafiti unapaswa kuwa jioni cha maendeleo, si zana ya kuimarisha kitambulisho cha kitaaluma au kupata fedha za ufadhili.
Mrejesho ni lazima. Kila utafiti unapaswa kumalizika kwa kutoa ripoti rahisi, mashauriano, au warsha kwa jamii.
Hatua zote za kitafiti zinapaswa kuzingatia maslahi ya jamii. Takwimu na maelezo yanayokusanywa lazima yaelezwe kwa jamii katika lugha rahisi.
Wafadhili wanapotoa fedha, wanapaswa kuhakikisha matokeo yanarudishwa kwa wenyeji.
Ni wakati wa kusema “Watafiti toeni mrejesho kwa jamii!” Matokeo ya utafiti hayapaswi kuishia kwenye ripoti, tasnifu, au mashubaka ya maktaba pekee. Jamii inapaswa kufaidika moja kwa moja.
Utafiti unaanza na jamii, unategemea jamii, na kimsingi lazima urejee jamii. Wenyeji wanastahili kuona thamani ya wakati wao, taarifa zao, na ushirikiano wao.
Bila mrejesho, utafiti unakuwa kazi tu ya kumfanikisha mtu kitaaluma na kupata fedha, lakini si chombo cha maendeleo ya kijamii. Hii ni dhahiri kuwa mfumo huu wa utafiti unapaswa kubadilika, ili kila kazi ya kitafiti iwe chombo cha ustawi na maendeleo halisi.
Kwa kuwa kutoa mrejesho ni sehemu ya uwajibikaji, njia zifuatazo zinaweza kutumiwa na watafiti ili yale waliyobaini kwenye utafiti yawafikiea wananchi.
Kwanza, watafiti wanaweza kuandaa mikutano ya hadhara au warsha katika maeneo husika. Hizi ziwe katika lugha rahisi na inayoeleweka kwa jamii, badala ya kutumia istilahi ngumu za kitaaluma.
Kupitia mikutano hiyo, wanajamii wanaweza kuuliza maswali na kutoa maoni yao kuhusu matokeo ya utafiti.
Pili, matumizi ya vyombo vya habari vya ndani kama redio za kijamii ni njia bora ya kufikisha ujumbe kwa watu wengi kwa wakati mmoja.
Vipindi maalum vinaweza kuandaliwa ambapo watafiti wanaeleza matokeo ya utafiti na kujibu maswali kutoka kwa wasikilizaji.
Tatu, watafiti wanaweza kuandaa vipeperushi, mabango au vijitabu vinavyofupisha matokeo muhimu ya utafiti kwa lugha rahisi. Hivi vinaweza kusambazwa katika vituo vya afya, shule, au ofisi za serikali za mitaa ili kuwafikia watu wengi zaidi.
Nne, ushirikiano na viongozi wa jamii ni muhimu. Viongozi hao wana ushawishi mkubwa na wanaweza kusaidia kufikisha taarifa kwa wananchi kwa njia inayokubalika na kueleweka kirahisi.
Mwisho, matumizi ya teknolojia kama mitandao ya kijamii na majukwaa ya kidijitali yanaweza kusaidia kufikisha mrejesho hasa kwa vijana. Video fupi, picha na ujumbe mfupi vinaweza kuvutia na kueleweka haraka.
Kwa kutumia njia hizi, watafiti wanaweza kuhakikisha kuwa jamii zinapata mrejesho wa tafiti, na matokeo hayo yanatumika kwa maendeleo halisi badala ya kubaki kwenye makabrasha yasiyosomwa.
