Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam leo tar 13/4/2026.
………….
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imefanikiwa kukamata jumla ya kilogramu 1,983.31 za dawa za kulevya katika operesheni maalum iliyofanyika mwezi Machi mwaka huu.
Mbali na kukamata dawa hizo, DCEA pia imekamata magari tisa, pikipiki 12 na bajaji moja zilizokuwa zikitumika katika usafirishaji wa dawa hizo. Aidha, mashamba ya bangi yenye ukubwa wa ekari 55.5 yameteketezwa huku watuhumiwa 77 wakikamatwa kuhusiana na matukio hayo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, alisema mafanikio hayo yametokana na operesheni kabambe inayolenga zaidi kudhibiti uzalishaji wa dawa za kulevya mashambani baada ya kupungua kwa mitandao ya dawa za viwandani.
Alieleza kuwa katika matukio mbalimbali ya ukamataji, eneo la Tegeta Kibo jijini Dar es Salaam lilikamatwa kilogramu 101.2 za mirungi zilizokuwa zimefichwa ndani ya basi la abiria aina ya Yutong la kampuni ya Abood, namba T 181 EMJ, lililokuwa likitokea Mombasa, Kenya kuelekea Dar es Salaam.
“Dawa hizo zilifichwa katika maeneo mbalimbali ya basi hilo ikiwemo ndani ya mfumo wa hewa (AC) kwa lengo la kukwepa kugundulika,” alisema Lyimo.
Aliwataja watuhumiwa waliokamatwa katika tukio hilo kuwa ni dereva wa basi hilo, Ramadhan Mohamed (52), kondakta Salma Sanga (26), pamoja na Twahilu Athuman (38), Mohamedy Mikidadi (37) na Ibrahim Mohamed (39).
Katika mkoa wa Pwani, alisema kilogramu 419.09 za mirungi zilikamatwa zikiwa zinasafirishwa kuelekea Dar es Salaam, huku mkoani Tanga kilogramu 32.95 za mirungi zikikamatwa zikiwa zimefichwa ndani ya mfuko uliochanganywa na maembe.
Katika tukio hilo la Tanga, mtuhumiwa Seif Omar (38), maarufu kwa jina la Haniwao na mkazi wa Mtaa wa Taifa Barabara ya 13, alikamatwa.
Aidha, mkoani Mwanza, kilogramu 52 za mirungi zilikamatwa katika kizuizi cha barabarani cha Magu pamoja na Bandari ya Mwanza South, zikiwa zinasafirishwa kwa kutumia gari aina ya Fuso lenye namba T 296 APA.
Dawa hizo zilikuwa zimefichwa katikati ya mizigo mingine ikiwemo mabelo ya nguo za mitumba. Dereva wa gari hilo, Hassan Hassan (37), mkazi wa Mahina Nyamagana, alikamatwa.
Kamishna Lyimo alisisitiza kuwa mamlaka hiyo itaendelea kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya mtu yeyote atakayebainika kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya bila kujali hadhi yake.
Aliongeza kuwa DCEA itaendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, taasisi nyingine pamoja na wananchi ili kudhibiti mianya yote inayotumiwa na wahalifu wa dawa za kulevya nchini.

